PWANI: Serikali imepanga kusafirisha nyama nje ya nchi kiasi cha tani elfu hamsini ifikapo mwako 2030.
Kwa sasa inasafirishwa nyama tani 14.000 kwenda nje ya nchi.
Shirika la Ranchi za Taifa (NARCO) katika kutekeleza azma hiyo ya Serikali imenunua Bulldozer kwa ajili kuondoa vichaka, kuboresha nyanda za malisho na kuchimba mabwawa ya maji ili kuboresha upatikanaji wa mifugo itakayotoa nyama bora ili kuweza kuchangia azma ya Serikali kusafirisha tani elfu 50 ifikapo 2030.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bulldozer mpya katika Ranchi ya Taifa ya Ruvu, mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa NARCO, Mohamedi Mbwana, alisema mashine hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 400 ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema bulldozer hiyo itatumika kuchimba visima vya maji, kuondoa vichaka vinavyozuia ukuaji wa malisho na kuweka mipaka ya ranchi ili kudhibiti uvamizi, hatua zitakazoongeza tija ya uzalishaji wa mifugo.


“Ununuzi wa bulldozer hii ni mwanzo wa mageuzi makubwa yanayolenga kuifanya NARCO kuwa kampuni ya mfano katika uzalishaji wa mifugo na bidhaa zake zenye ushindani wa kikanda na kimataifa,” amesema Mbwana.
Aliongeza kuwa NARCO itaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya mifugo, kuanzia uzalishaji wa mifugo na malisho, uchakataji wa nyama hadi masoko ya kimataifa.
Mbwana pia aliwahimiza wafugaji kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia uwekezaji unaoendelea katika sekta ya mifugo ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NARCO, Balozi Dkt. Aziz Ponary Mlima, alisema bulldozer hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji katika ranchi za taifa na kuongeza ufanisi wa shughuli za ufugaji.
Alibainisha kuwa NARCO itaendelea kuwawezesha wawekezaji waliopo ndani ya ranchi kwa kuwapatia huduma mbalimbali, ikiwemo ukodishaji wa mitambo, ili kuongeza uzalishaji na mapato ya Serikali.
Aidha, aliwahimiza wafugaji kuwekeza katika matumizi ya mbegu bora za mifugo, madume bora, teknolojia ya uhimilishaji na matumizi ya viini tete ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mifugo.
Naye Mwenyekiti wa Wawekezaji wa Ranchi ya Ruvu, Mapili Kisanjo, aliipongeza Serikali kwa ununuzi wa mashine hiyo, akisema itasaidia kusafisha maeneo yenye vichaka na kuboresha malisho.
Hata hivyo, aliomba Serikali kuhakikisha upatikanaji wa chanjo za mifugo katika ranchi hizo ili kuwawezesha wafugaji kupata huduma kwa urahisi na kuongeza tija ya uzalishaji.





