HomeHabariMasauni ataka mifumo endelevu ya udhibiti wa taka Dar

Masauni ataka mifumo endelevu ya udhibiti wa taka Dar

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amezitaka mamlaka za Dar es Salaam kuweka mifumo endelevu ya ukusanyaji na utunzaji wa taka ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kupunguza athari za mvua.

Masauni amesema usafi wa jiji haupaswi kutegemea maagizo ya viongozi wa juu, bali uwe sehemu ya utendaji wa kila siku wa taasisi na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira.

Amesema hayo Oktoba 11, 2026, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira katika Mto Ng’ombe, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa Dar es Salaam ni sura ya nchi, hivyo viongozi katika ngazi zote wana wajibu wa kuhakikisha jiji linakuwa safi na mazingira yanalindwa wakati wote.

Masauni amesema licha ya changamoto za upangaji wa makazi katika baadhi ya maeneo, mamlaka zinapaswa kuimarisha udhibiti wa utupaji holela wa taka na kuweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji wake.

Ameonya kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais haitakubali uzembe katika utekelezaji wa shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira, akizitaka taasisi na halmashauri kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji.

Amesema taka zinaweza kuwa chanzo cha mapato na ajira kwa wananchi ikiwa zitakusanywa na kuchakatwa kwa utaratibu unaofaa, badala ya kutupwa ovyo na kuhatarisha afya za watu na mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema wilaya hiyo inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira.

Mtambule amesema wakazi wanaoishi karibu na Mto Ng’ombe wameelekezwa kuondoka katika maeneo hayo ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua, huku zoezi la kubomoa nyumba katika maeneo husika likiwa limeanza.

Ameongeza kuwa ukusanyaji wa taka na juhudi za kuhamasisha jamii kulinda mazingira vinaendelea, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kudhibiti uchafuzi na kupunguza athari za mvua.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments