Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema vitambulisho vya Taifa 6,308 vilivyochapishwa kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar bado havijachukuliwa, hali inayoweza kuwasababishia usumbufu wanapohitaji huduma zinazotaka kitambulisho hicho.
Katambi amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, akiwataka wananchi waliopata ujumbe kuwa vitambulisho vyao vimekamilika kwenda kuvichukua.
Amesema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeweka mifumo ya kiteknolojia ya kutuma ujumbe kwa wananchi kuwajulisha kuwa vitambulisho vyao vimekamilika, lakini baadhi yao bado hawajaitikia wito huo.
Katambi ameipongeza NIDA kwa kusajili Watanzania 943,284, huku akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kukamilisha mchakato wa kupata vitambulisho vyao kwa kuvichukua baada ya kuchapishwa.
Amesema kitambulisho cha Taifa ni muhimu katika kupata huduma mbalimbali, hivyo wananchi hawapaswi kutegemea namba ya NIDA pekee wakati vitambulisho vyao tayari vimekamilika.
“Ni kweli mtu anaweza kuwa na namba ya NIDA, lakini kuna wakati itakapohitajika huduma fulani utatakiwa kuwa na kitambulisho chenyewe. Tusisubiri mpaka tukihitaji ndipo tuanze kukitafuta,” amesema.
Ameonya kuwa Serikali inaweza kuweka utaratibu wa kutokubali namba ya NIDA pekee katika baadhi ya huduma zinazohitaji kitambulisho halisi, akiwataka wananchi kuchukua vitambulisho vyao mapema ili kuepuka usumbufu.
Katika hatua nyingine, Katambi amesema Serikali inafikiria kuweka utaratibu wa kutoza faini kwa wananchi watakaochelewa kuchukua vitambulisho vyao baada ya kupewa taarifa kuwa vimekamilika.




