Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na taasisi za fedha za kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), unaendelea kuimarika huku Serikali ikiangazia uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, kilimo na nishati.
Omar ameyasema hayo Oktoba 12, 2026, alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk. Ndiame Diop, kando ya Mikutano ya Mwaka ya IMF na Benki ya Dunia inayofanyika Bangkok, Thailand.
Amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua, akieleza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu ukuaji umefikia asilimia 6.3. Aidha, amesema ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi vimeendelea vizuri, huku mfumuko wa bei ukiwa ndani ya wigo wa asilimia tatu hadi tano.

Kuhusu ushirikiano na Benki ya Dunia, Omar amesema taasisi hiyo inafadhili miradi 33 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 8.8 katika sekta mbalimbali, zikiwemo viwanda, elimu, afya, kilimo na mifumo ya hifadhi ya jamii kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Amesema miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa ushirikiano huo inajumuisha uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa Reli ya Kati (MGR) na Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na miradi ya nishati inayolenga kuunganisha gridi ya taifa na Zambia.
Kuhusu IMF, Omar amesema Tanzania imekamilisha programu zilizokuwa zikiendelea na sasa inafanya tathmini ya ndani kubaini mahitaji yake kabla ya kuamua kuhusu makubaliano mapya na taasisi hiyo.
Katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2026, Tanzania ilinufaika na programu mbili za IMF zilizolenga kuimarisha uchumi na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Programu hizo zilihusisha Mpango wa Upatikanaji wa Mikopo Nafuu (ECF) na Mpango wa Ustahimilivu na Uendelevu (RSF).




Kwa upande wake, Diop ameipongeza Tanzania kwa hatua za maendeleo ya kiuchumi na kuahidi kuwa Benki ya Dunia itaendelea kuwa mshirika muhimu katika kufadhili miradi ya kimkakati ya Serikali na mipango ya maendeleo ya kikanda.
Ametaja maeneo yatakayoendelea kupewa kipaumbele kuwa ni nishati, elimu, miundombinu ya reli, ikiwemo Reli ya Kati, msaada kwa kaya zenye kipato cha chini kupitia TASAF, maendeleo ya rasilimali watu na miradi ya kikanda.
Mazungumzo hayo yanafanyika katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa kutafuta rasilimali za kugharamia miradi ya maendeleo na kuimarisha uchumi.





