Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa kundi la tano, yakiwahusisha jumla ya askari wapya 370, yenye lengo la kuwaandaa kikamilifu kutekeleza majukumu yao katika kulinda na kusimamia rasilimali za misitu nchini.
Mafunzo hayo, yanayoendelea mkoani Morogoro kuanzia Novemba 13, 2025, yamelenga kuwajengea uwezo watumishi hao wapya kuhusu utendaji bora, uadilifu, na utii wa sheria kabla ya kuanza kazi rasmi katika vituo vyao mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, Naibu Kamishna wa TFS, Emmanuel Wilfred, alisema hatua hiyo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya watumishi kabla ya kuingia kazini.




“Watumishi hawa wanakwenda moja kwa moja kwenye utekelezaji wa majukumu ya TFS. Ni muhimu wakapata uelewa sahihi wa sheria, taratibu za utumishi wa umma na maadili ya kazi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Wilfred.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo yamejikita katika maeneo muhimu ikiwemo usimamizi wa fedha za umma, matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki, haki za watuhumiwa, na mbinu za kuongeza ufanisi wa kazi za kila siku.
Wilfred aliongeza kuwa TFS inaendelea kuboresha mifumo yake ya kiutendaji ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji, na matumizi bora ya rasilimali.
“Tunatarajia kuona matokeo chanya kupitia maarifa mliyopata. Ni wajibu wenu kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka washiriki hao kutumia mafunzo hayo kama nyenzo ya kuongeza tija, ubunifu na ufanisi, ili kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya misitu na mazingira kwa ujumla.








