Tuesday, March 3, 2026
spot_img
HomeHabariWaziri Ndejembi azindua Mita Janja za TANESCO

Waziri Ndejembi azindua Mita Janja za TANESCO

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameongoza uzinduzi wa Mita Janja (Smart Meters) za TANESCO, mfumo mpya wa kisasa unaolenga kuboresha utoaji wa huduma za umeme nchini na kuongeza ufanisi kwa Shirika na wateja wake.

Akizungumza katika hafla hiyo  iliyofanyika leo, Waziri Ndejembi alitoa pongezi  kwa Shirika la TANESCO kwa hatua kubwa ya kimapinduzi waliyoifikia katika maboresho ya huduma kwa umma.

“Leo tumekutana kwa tukio muhimu, kubwa na la kihistoria, lenye alama chanya ya mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma ya umeme nchini. Niwapongeze TANESCO kwa hatua hii ya kuleta mageuzi makubwa katika kuboresha uzoefu wa mteja,” amesema.

Ameongeza kuwa uzinduzi wa Mita Janja ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wananchi wanapata umeme bora, wa uhakika na unaoendana na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa.

Waziri Ndejembi amekumbusha changamoto ambazo wateja walikuwa wanakutana nazo kwa kutumia mita za zamani, ikiwemo kushindwa kuona matumizi ya umeme kwa wakati halisi, ugumu wa kupanga bajeti, pamoja na hitilafu mbalimbali kama tokeni kushindwa kuingia, kupotea kwa kumbukumbu au kuharibika kwa rimoti za kuingiza tokeni.

Ameeleza kuwa baadhi ya mita zilikwekwa katika maeneo magumu kufikika, hali iliyowalazimu wateja kupanda ngazi au stuli kila wanaponunua umeme, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa hasa wakati wa dharura.

“Rimoti za zamani zilikuwa kero kwa wateja. Zilikuwa zinavunjika, kuharibika au kuvuja betri na hata wakati mwingine kushindwa kuingiza tokeni kabisa, hasa usiku. Haya yote yalikuwa ni mzigo kwa wananchi,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri, kuanzishwa kwa Mita Janja ni matokeo ya uamuzi wa Serikali na TANESCO kupambana na changamoto hizo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Kupitia mita hizo mpya, wananchi wataweza:

  • 📌Kuingiza umeme popote walipo bila kulazimika kufika nyumbani.
  • 📌Kufuatilia matumizi yao kwa muda halisi kupitia mfumo mahiri.
  • 📌Kupata taarifa za kuisha kwa umeme kwa wakati kupitia kiashiria (alert).

Kwa upande wa TANESCO, mita hizi zitasaidia kubaini wizi wa umeme, kutambua uharibifu wa mita, na kupunguza upotevu wa nishati kwa wakati halisi, hivyo kuimarisha mapato ya shirika na kulinda fedha za Serikali.

“Naipongeza TANESCO kwa kuanza kufunga mita hizi kwenye maeneo mbalimbali nchini. Wateja wanaozipata wameanza kutoa mrejesho mzuri, jambo linalotupa hamasa ya kusonga mbele,” amesema.

Waziri Ndejembi pia amezungumzia maboresho mengine ndani ya shirika, yakiwemo:

  • 📌Mfumo wa kisasa wa maombi ya kuunganishiwa umeme (Nikonekt).
  • 📌Kituo kipya cha kisasa cha kupokea miito ya simu (Unified Call Centre).
  • 📌Mfumo wa huduma kwa mteja kupitia chatbot ya JISOti.

Amesema pamoja na uwekezaji huo, TANESCO ina wateja zaidi ya milioni 5.6, hivyo mabadiliko ya mita yatafanyika kwa awamu kadri ya mpango wa Shirika.

📍Maelekezo kwa TANESCO

Katika hotuba yake, Waziri Ndejembi ameielekeza TANESCO kufanya yafuatayo:

  • 📌Kusambaza Mita Janja katika mikoa yote bila kuchelewa, bila gharama kwa wateja wenye uhitaji wa haraka.
  • 📌Kuhakikisha wateja wote wapya wanawekewa Mita Janja.
  • 📌Kufanikisha ufungaji wa mita kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
  • 📌Kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi na faida za mita hizo.
  • 📌Kuboresha kila mwaka mfumo unaoziendesha Mita Janja (AMI).
  • 📌Kuimarisha mawasiliano na wateja na kuongeza ubunifu katika huduma.

“Watanzania wanahitaji umeme wa uhakika na huduma bora. Nawataka TANESCO mfanye kazi kwa weledi na ubunifu ili kuendana na kasi ya mahitaji ya nchi,” amesisitiza.

📍Pongezi kwa Wadau na Timu ya TANESCO

Waziri Ndejembi ameipongeza Bodi ya TANESCO, Menejimenti, wataalam wa TEHAMA, kitengo cha usimamizi wa mita, na vitengo vyote vilivyohusika na mradi huu kwa zaidi ya miaka 18.

“Kwa dhati kabisa nawapongeza wote. Mmeweka historia mpya ya kuleta suluhisho la kisasa kwa wateja. Pia nawapongeza wadau wote wa ndani na nje ya nchi walioshiriki kwenye utafiti, majaribio na uwekezaji huu,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa teknolojia hii ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo thabiti, wa kidijitali na wa kisasa wa usimamizi wa umeme.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments