Airtel Tanzania imeendeleza ushirikiano wake na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kupitia makubaliano mapya ya Awamu ya 10, hatua inayolenga kupanua na kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini.
Hafla ya utiwaji saini imefanyika Desemba 5, 2025, ikihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ambaye amepongeza jitihada zinazoendelea za serikali na sekta binafsi katika kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Katika awamu hii, Airtel Tanzania inatarajiwa kujenga minara 132 kati ya 201 itakayojengwa nchi nzima. Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma za mawasiliano za kuaminika, za kisasa na za gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Waziri Kairuki aliisifu UCSAF na kampuni za simu kwa kazi wanayoifanya kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na maendeleo ya teknolojia.

Alisema:
“Naipongeza Bodi na Menejimenti ya UCSAF kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa ubora na gharama nafuu. Pia nawapongeza watoa huduma wote kwa ushirikiano mkubwa mnaouonyesha kwa Serikali ili kuhakikisha huduma zinaendelea kuwa bora na zenye tija kwa wananchi.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Mohamed Hamis Abdullah, alisisitiza umuhimu wa mradi huo, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ili kufikia malengo ya upatikanaji jumuishi wa mawasiliano.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema utekelezaji wa awamu hii unathibitisha dhamira ya Airtel katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali nchini.

Amesema:
“Kupitia mradi huu wa Awamu ya 10, Airtel inajivunia kujenga 65% ya minara yote—sawa na 132 kati ya 201. Hii inaonyesha kujitolea kwetu katika kupanua mtandao na kuhakikisha jamii nyingi zaidi zinanufaika na huduma za kisasa za mawasiliano.”
Airtel Tanzania imeeleza kuwa itaendelea kuboresha huduma zake kwa Watanzania kote nchini, ili kuhakikisha fursa za kidijitali zinawafikia wananchi wa mijini na vijijini.





