Wednesday, March 25, 2026
spot_img
HomeHabariBalozi CP Kaganda aungana na nchi za SADC kuadhimisha Siku ya Ukombozi...

Balozi CP Kaganda aungana na nchi za SADC kuadhimisha Siku ya Ukombozi Kusini mwa Afrika

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimeadhimisha Siku ya Ukombozi ya Kusini mwa Afrika kwa shughuli mbalimbali zilizofanyika jijini Harare, Zimbabwe zikiwa na lengo la kuenzi historia ya harakati za ukombozi na kuhamasisha uhifadhi wa urithi wa kihistoria.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kuanzia Machi 23 hadi 25, ambapo yaliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, wanahistoria na vijana kutoka mataifa tofauti ya ukanda huo, Kaulimbiu kuu ilijikita katika kuimarisha umoja, kuthamini historia ya ukombozi, pamoja na kulinda maeneo na simulizi za kihistoria.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, alisisitiza umuhimu wa kizazi cha sasa kujifunza historia ya mapambano ya uhuru ili kuendeleza mshikamano na maendeleo ya kudumu katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Katika hotuba yake, alieleza kuwa ni jambo la fahari kubwa kusimama mbele ya hadhira hiyo, si tu kama Kaimu Mkuu wa Kundi la Mabalozi, bali pia kama mwakilishi wa kikanda kutoka eneo ambalo historia yake imejengwa juu ya misingi ya uthabiti, umoja na mshikamano wa watu wake.

Aidha, katika kile kilichoelezwa kama “Heritage Village”, washiriki walipata fursa ya kushuhudia maonesho ya utamaduni ikiwemo muziki wa asili, ngoma za jadi na vyakula vya kienyeji pamoja na maonesho ya kihistoria yaliyobainisha hatua mbalimbali za harakati za ukombozi pamoja na programu maalum za elimu kwa vijana.

CP Kaganda aliongeza kuwa maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika yanawakumbusha watu juu ya ujasiri na kujitolea kwa wanaume na wanawake wengi waliopambana kwa dhati dhidi ya ukoloni, ukandamizaji na dhuluma.

Alisisitiza kuwa siku hiyo si tu kumbukumbu ya yaliyopita, bali pia ni wito wa kuendeleza maadili na misingi ya uhuru, mshikamano na haki kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Siku ya Ukombozi ya Kusini mwa Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Machi, ikiwa na lengo la kukumbuka mchango wa harakati za ukombozi zilizowezesha nchi nyingi za ukanda huo kupata uhuru.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments