Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda amesema kwa sasa mamlaka hiyo imejipanga kutoa huduma kwa Saa 24 katika Bohari za mafuta(Depot) huku akisisitiza uwepo wa udhibiti katika udanyanyifu kutoka kwa watoa huduma hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam wakati wa ziara ya kutembelea vituo vya kuhifadhia mafuta (Depot), Mwenda kama ilivyo kwa Mameneja wa ‘Depot’ alizotembelea amesema Tanzania ina mafuta ya kutosha na kwamba changamoto zilizoripotiwa hazihusiani na uhaba wa mafuta hayo.
Akitembelea maghala ya kuhifadhia mafuta ya Camel, Mount Meru pamoja na Moil Energies, Mwenda amesema amejiridhisha na uwepo wa mafuta ya kutosha katika maeneo hayo na mengine huku akiwasisitiza wafanyabiashara hiyo kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ufasaha.

”Kama ambavyo Serikali imesema kuwa hakuna upungufu wa mafuta, TRA pia tunasisitiza kuna mafuta ya kutosha nchini hivyo tunawaomba watoa huduma hiyo kuzingatia taratibu za uuzaji wa mafuta hayo” amesema Mwenda
Aidha amewataka wauzaji wa mafuta hayo kuhakikisha wanashirikiana na Mamlaka hiyo ili kuwezesha huduma ya utoaji mafuta kwenye vituo hivyo inatolewa kwa Saa 24 ili kurahisisha kazi ya usambazaji wa mafuta hayo.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu wa TRA amesema kwa sasa wamekuja na utaratibu mpya unaohusisha ulipaji Kodi wa mafuta ya vyombo vya moto kabla ya kuanza kuuzwa nchini huku yale yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi utaratibu wake wa kodi pia ukizingatiwa.
Akitolea ufafanuzi kuhusu kuhusu suala hilo Kamishna wa Forodha kutoka TRA Juma Hassan amesema kupitia kwa utaratibu huo mpya ambao umepokelewa vizuri pia na wauzaji wa mafuta kwa kiasi kikubwa kutasaidia kuondoa udanganyifu na kuiwezesha Serikali kukusanya kodi kwa ufasaha
”Kimsingi utaratibu ni kwamba mafuta ya ndani yanalipiwa kodi kabla hayajaingia hayajauzwa huku tukifuatilia mauzo ya mafuta hayo, na mafuta yale yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi utaratibu huu utahakikisha hayarudishwi tena nchini pasipo kulipiwa Kodi” amesisitiza Juma
Aidha amezitaka vyote kuhakikisha mafuta yanayobaki nchini yanatoka utaratibu wa mauzo yake unarekodiwa katika vituo vyote vya mauzo, na mafuta yale ambayo yanasafirishwa yanafuata utaratibu kabla hayajasafirishwa .
Kwa upande wao Mameneja wa vituo vya kuhifadhia mafuta vya Camel Oil, Mount Meru pamoja na Moil Energies, pamoja na kumshukuru Kamishna wa TRA kwa kuwatembelea na kuona utendaji wao wa kazi, wamesema wameupokea kwa mikono miwili uwepo wa mfumo mpya wa udhibiti wa uuzaji wa mafuta.

Msimamizi wa kituo cha kuhifadhia mafuta cha Mount Meru Omari Yusufu amesema utaratibu mpya wa uuzaji mafuta ya Dizel na Petroli uliowekwa na TRA umeondoa changamoto ya uchepushaji mafuta na kuhakikisha kila mzigo u aotoka kwenye vituo hivyo unakwenda mahala ulipokusudiwa.
Meneja wa Moil Energies Sajad Habib Rai, amesema kuna mafuta ya kutosha katika maghala yao na kusisitiza kuwa wao kama watoa huduma wanafanya kazi Kwa kuhakikisha wanatoka huduma kwa kila mfanyabiashara kwa kuzingatia misingi ya uwazi na ukweli.
Ameishukuru TRA kwa kufanya nao kazi nje ya muda wa kawaida ikiwemo mpaka saa 24 pale panapokuwa na uhitaji mkubwa ili kuhakikisha shehena ya mafuta inatoka kwenye maghala na kuungia sokoni.
Kwa upande Meneja Uhifadhi na usambazi kutoka Kampuni ya Camel Oil Omary Abeid amesema wana akiba ya kutosha mahali hapo huku wakizingatia taratibu za uuzaji wa mafuta hayo kwa haki kwa wafanyabiashara wote.
“Kama mtu huwa anaagiza lita 1,000 kwa mwezi atauziwa kiwango hichohicho, maana kuna wengine wanataka kununua kiwango kikubwa zaidi sisi hatukubali kuwauzia kiwango hicho bali tunaangalia taarifa zao za awali ili na wengine wapate” amesema Abeid
Amesema kutokana na mahitaji ya kiasi kikubwa cha mafuta kutoka baadhi ya wafanyabiashara waliweka utaratibu wa kuuza mafuta hayo ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata mafuta hayo.




