Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) imefuzu kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 52, kufuatia ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Jamaica katika fainali ya mchujo wa mabara iliyochezwa Uwanja wa Guadalajara, Mexico.
Bao la ushindi lilifungwa katika dakika za nyongeza na Axel Tuanzebe, ambaye kabla ya mchezo alieleza kuwa hiyo ndiyo mechi kubwa zaidi kuwahi kucheza katika maisha yake ya soka. Tuanzebe, aliyezaliwa Bunia mashariki mwa DR Congo, ameandika historia mpya kwa nchi yake kupitia ushindi huo muhimu.
Katika dakika 90 za kawaida, mshambuliaji wa Leopards Cédric Bakambu alifunga mabao mawili yaliyokataliwa kwa madai ya kuotea, hali iliyosababisha mchezo kuamuliwa katika dakika 30 za nyongeza.
Hatimaye, Tuanzebe alitumia vyema kona iliyopigwa na Brian Cipenga na kuusukuma mpira wavuni kwa kifua katika dakika ya 100, baada ya mpira kumgusa kidogo beki wa Jamaica Joel Latibeaudiere kabla ya kumfikia.
Shangwe zilisimama kwa muda wakati waamuzi walipokuwa wakikagua tukio hilo kupitia VAR kwa uwezekano wa mpira kugusa mkono, lakini uamuzi ulithibitisha kuwa hapakuwa na kosa.
Kwa upande wa Jamaica, waliokuwa wakilenga kurejea Kombe la Dunia kwa mara ya pili tangu ushiriki wao wa mwaka 1998 nchini Ufaransa, walishindwa kutengeneza nafasi za kutosha kusawazisha bao.
Kwa ushindi huo, DR Congo imepangwa katika Kundi K la mashindano hayo yatakayoshirikisha timu 48, ambapo wataanza kampeni yao kwa kucheza dhidi ya Ureno Juni 17 mjini Houston, kabla ya kukutana na Colombia na Uzbekistan.




