HomeMichezoCRDB Bank Foundation yatenga milioni 400/- Imbeju – Ndondo Cup

CRDB Bank Foundation yatenga milioni 400/- Imbeju – Ndondo Cup

Mdhamini mkuu wa msimu wa 13 wa Imbeju – Ndondo Cup 2026, taasisi ya CRDB Bank Foundation, amesema wametenga zaidi ya shilingi milioni 400 zitakazotumika kuendesha ligi hiyo inayowahusisha vijana kutoka mtaani zikiwamo zaidi ya shilingi milioni 100 zitakazotolewa kama zawadi kwa timu, wachezaji na mashabiki.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ligi hiyo inayotekelezwa mpaka ngazi ya mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa amesema msimu huu unaleta fursa juu ya fursa kwa kila mdau wa Imbeju – Ndondo Cup.

“Mashindano ya Imbeju – Ndondo Cup 2026 yataanzia mashinani hadi ngazi ya mkoa. CRDB Bank Foundation imewekeza jumla ya shilingi milioni 400 ambazo zinajumuisha gharama za uendeshaji pamoja na zawadi. Bingwa wa mashindano haya atapata shilingi milioni 30 na mshindi wa pili atapata shilingi milioni 15 na kwenye kila hatua timu inayofuzu itapewa kiasi cha fedha. Pia, kutakuwa na zawadi kwa mchezaji bora, mfungaji bora, beki bora na kipa bora wa Imbeju Ndondo Cup 2026 pamoja na shabiki ua kikundi maahiri kwa kushangilia,” amesema Tully.

Katika kila mechi, Tully amesema mchezaji bora wa mechi (man of the match) atapata shilingi 100,000 na shabiki mahiri pia atapata shilingi 100,000. Fedha hizi zitawekwa kwenye Akaunti ya Imbeju ya kila muhusika hivyo kutoa fursa juu ya fursa hali inayotimiza kaulimbiu ya Imbeju – Ndondo cup 2026 isemayo ‘Jiongeze.’

Na msimu wa michuano utakapokamilika, mchezaji bora atajinyakulia shilingi milioni 3 huku golikipa na beki bora wakipata shilingi milioni 1 kila mmoja. Zawadi hizi zote, Tully amesema zinakusudia kufungua fursa kwa timu na wachezaji kutoka mtaani kuianza vyema safari yao ya kujijenga kiuchumi.

Mkurugenzi amesema kuwa CRDB Bank Foundation inathamini sana umahiri ndio maana imetoa kipaumbele kwa kila atakayeonyesha uwezo wa juu ndani ya uwanja na jukwaani walipo watazamaji kwa kumtambua mshabiki au kikundi cha mashabiki watakaonyesha upekee katika kushangilia.

Akizindua msimu huu mpya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Saad Mtambile ameipongeza CRDB Bank Foundation kwa jitihada za kuwainua vijana, wanawake na makundi maalumu kupitia Programu yake ya Imbeju akisema inaleta mapinduzi makubwa katika kuboresha maisha ya wananchi.

“Kwa zawadi zitakazotolewa, naamini ndoto ya kuifanya iMbeju – Ndondo Cup itakuwa ligi yenye mvuto nchini. Mara nyingi CRDB Bank Foundation mmekuwa mstari wa mbele kuboresha maisha ya wananchi, serikali inajivunia jitihada zenu, hongereni sana. Ligi hii kwa sasa inatambuliwa mpaka na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye huwa anatoa zawadi ya bao la mama,” amesema Mheshimiwa Mtambile.

Katika msimu huu mpya wa IMBEJU – Ndondo Cup ambao taasisi ya CRDB Bank Foundation inashirikiana na waandaaji wa michuano hiyo, Shadaka Sports, wamedhamiria kuhakikisha vijana wote wanaoshiriki mashindano haya wanapata maarifa, ujuzi na nyenzo zitakazowasaidia kujenga maisha bora hata nje ya uwanja.

Katika msimu huu, vijana watapata elimu ya fedha na kufunguliwa Akaunti ya Imbeju kuwawezesha kusimamia mapato yao yatokanayo na vipaji vyao ili waweze kujenga uchumi imara, mafunzo ya uwekezaji na ujasiriamali pamoja na mafunzo ya ubunifu na fursa za uchumi wa kisasa.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mratibu wa Imbeju – Ndondo Cup kutoka kampuni ya Shadaka Sports, Yahaya Mohammed amesema michezo ni chombo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na michuano hii imeendelea kuthibitisha kwamba vipaji vikipewa nafasi vinaweza kubadilisha maisha ya vijana wengi nchini.

“Uzinduzi huu wa Imbeju – Ndondo Cup 2026 unaleta matumaini mapya kwa maelfu ya vijana wanaosubiri kuonyesha uwezo wao katika soka. Kwa vijana wote watakaoshiriki mashindano haya, waione Imbeju – Ndondo Cup kama jukwaa la kuonyesha nidhamu na kufungua milango ya mafanikio makubwa zaidi,” amesema Mohammed.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments