Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kufuata sera ya kutofungamana na upande wowote, akisisitiza Taifa hilo litaendelea kushirikiana na washirika mbalimbali duniani licha ya mabadiliko ya mazingira ya uchumi wa dunia.
Msisitizo huo wa Rais Samia, unajibu swali la Mwandishi wa Kituo kimoja cha Televisheni cha Urusi, aliyeuliza Tanzania inawezaje kuhusiana na kushirikiana na mataifa tofauti, katika kipindi ambacho mazingira ya uchumi wa dunia yamebadilika.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika alipokuwa ziarani nchini Urusi, Rais Samia amesema Tanzania haifungamani na upande wa nchi yoyote kati ya zinazogombana, kwa kuwa inafuata sera ya kutofungamana na upande wowote na kulinda maslahi ya Taifa.
“Tanzania inafuata misingi ya kutofungamana na upande wowote. Kwa hiyo adui wa rafiki yetu si adui wetu, na rafiki wa adui yetu si adui wetu,” amesema.
Amesema Tanzania inaendelea kushirikiana na washirika mbalimbali wa kimataifa, wakiwemo wawekezaji kutoka Asia, Ulaya na Marekani, wote wakifanya kazi ndani ya mfumo wa sheria na sera za nchi zinazolenga kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, amesisitiza wawekezaji wote wanahudumiwa kwa usawa chini ya sheria na sera za taifa, zilizowekwa kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa thabiti na yanayotabirika.
Amesema mtazamo huo wa Tanzania unabaki kuwa uleule kwa washirika wote, ikiwemo Urusi, ambayo ina uhusiano nayo unaodumu kwa zaidi ya miaka 60.




