Biashara ndogo na za kati (SMEs) zinachangia takribani asilimia 95 ya biashara zote nchini Tanzania na huzalisha karibu asilimia 35 ya Pato la Taifa (GDP), huku zikiajiri zaidi ya nusu ya nguvu kazi ya taifa. Kwa mujibu wa ripoti za Benki ya Dunia, zaidi ya asilimia 90 ya SMEs
zinaendesha shughuli zake katika sekta isiyo rasmi. Hata hivyo, kwa wengi wao, gharama za usafiri na usafirishaji wa mizigo zimeendelea kuwa miongoni mwa mzigo mkubwa wa uendeshaji.
Kwa mfano, eneo la kibiashara la Kariakoo, ambalo mapato yake ya kodi kupitia TRA katika mwaka wa fedha 2024/2025 yalikaribia wastani wa Shilingi milioni 400 kwa siku, linategemea kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mizigo kutoka nje ya nchi na usambazaji wa bidhaa ndani ya
Dar es Salaam na mikoa mingine. Aidha, zaidi ya biashara 5,000 zisizo rasmi hutegemea harakati za wateja au uwasilishaji wa oda kupitia huduma za ride-hailing.
Kwa SMEs za huduma kama ushauri wa kitaalamu, udalali na mashirika mbalimbali, usafiri ni hitaji la kila siku. Ziara za wateja, mikutano, mawasilisho na matukio huongeza gharama za uendeshaji, hasa katika miji kama Dar es Salaam ambako msongamano na mabadiliko ya bei
za mafuta huongeza gharama za kila siku.
Katika mazingira haya, ride-hailing imekuwa mbinu ya kupunguza gharama. Zaidi ya asilimia 70 ya biashara zilizosajiliwa na Bolt Tanzania ni SMEs, zikionyesha utegemezi mkubwa kwa suluhisho la usafiri linalobadilika kulingana na matumizi. Tofauti na kumiliki magari ambayo
huambatana na gharama za matengenezo, bima na mafuta, ride-hailing huruhusu biashara kulipa kwa safari zilizofanyika pekee.
Kupitia Bolt for Business, kampuni hupata zana za kidijitali za kusimamia malipo, kufuatilia matumizi ya safari kwa wakati halisi na kuandaa ripoti za gharama, hatua inayosaidia kupunguza upotevu wa fedha na kuongeza uwajibikaji.
“SMEs ndio uti wa mgongo wa sekta binafsi Afrika Mashariki. Kwa wengi wao, usafiri nafuu na wenye ufanisi ni tofauti kati ya kusalia palepale na kukua,” anasema Milu Kipimo, Meneja wa Kanda na Mkuu wa Bolt for Business Afrika.
Kadri miji inavyozidi kupanuka na gharama za mafuta kubadilika, suluhisho za usafiri wa kidijitali zinaendelea kuwa nguzo muhimu ya ushindani na ufanisi wa SMEs nchini Tanzania.




