MWANZA, JULAI 26, 2026 — Benki ya CRDB imezindua rasmi programu ya mafunzo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), inayojulikana kama SME Toolkit, ikiwa na lengo la kuwawezesha kuongeza maarifa, ujuzi na uwezo wa kusimamia biashara zao kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo jijini Mwanza, Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Ronald Melkiory, amesema SME Toolkit imeandaliwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Fedha ya Maendeleo ya Ufaransa (PROPARCO) kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kukuza na kuimarisha biashara zao.
Amesema biashara ndogo na za kati zina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, zikichangia zaidi ya asilimia 95 ya biashara zote nchini na takribani asilimia 27 ya Pato la Taifa.




Hata hivyo, amesema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa mitaji, masoko na ushauri wa kitaalamu.
“Kwa kutambua umuhimu wa sekta hii na changamoto zake, Benki ya CRDB tumeandaa programu hii ya SME Toolkit ili kuwawezesha wafanyabiashara kujenga misingi imara ya biashara, kuboresha usimamizi wa fedha na kumbukumbu za biashara, pamoja na kutumia teknolojia na fursa za kidijitali kukuza shughuli zao,” amesema Melkiory.
Kupitia programu hiyo, wafanyabiashara watapatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali, yakiwemo utambuzi wa fursa za biashara, urasimishaji wa biashara, usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu, utafutaji wa masoko, matumizi ya teknolojia na udhibiti wa vihatarishi vya biashara.

CRDB imeeleza kuwa programu hiyo itatekelezwa katika wilaya 35 zilizopo kwenye mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku ikilenga kuwafikia wafanyabiashara wasiopungua 10,000.
Kwa mujibu wa benki hiyo, mpango huo unalenga kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati, kuongeza ajira rasmi na kukuza uzalishaji katika uchumi wa taifa.

Baada ya uzinduzi huo, CRDB iliendesha semina maalum jijini Mwanza iliyowakutanisha wafanyabiashara kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupata mafunzo kuhusu namna ya kuimarisha na kukuza biashara zao.
Benki hiyo imewahimiza wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini kote kujitokeza kushiriki katika semina za SME Toolkit zitakazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini, kwa mujibu wa ratiba itakayotangazwa.





