Kituo cha kupandikiza mimba cha Kairuki Green IVF (KGIVF), kilichoko Bunju A jijini Dar es Salaam kimefikisha jumla ya watoto 160 tangu kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk Clementina Kairuki, wakati akizungumzia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya IVF ambayo huadhimishwa kila tarehe 25 Julai kila mwaka.
Alikuwa akizungumza na wasanii wa JUAKALI waliotembelea kituo hicho kujifunza namna kinavyofanya shughuli zake za kupandikiza mimba na kusaidia familia zenye changamoto ya uzazi.
Dk Clementina alisema tarehe 25 Julai imepangwa kuwa siku ya IVF duniani kwani ndiyo siku ambayo mtoto wa kwanza alipatikana kwa njia ya upandikizaji mimba ambaye kwa sasa anamiaka 47.
“Tunawapongeza sana watu waliogundua hii IVF kwasababu haikuwa rahisi kwani waligundua baada ya kujaribu mara nyingi sana, walijaribu karibu mara 103 ndipo wakafanikiwa mtoto wa kwanza akazaliwa, hata magazeti ya wakati ule Uingereza yanaonyesha habari zote ziliandika tukio hilo,” alisema

Alisema tangu kuzaliwa kwa mtoto huyo wa kwanza teknolojia ya upandikizaji mimba imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na inafanyika kwa njia za kisasa Zaidi kuliko ilivyokuwa ikifanyika miaka ya zamani.
“Mpaka kufikia juzi tarehe 23 Julai tulikuwa na watoto 158 lakini jana wamezaliwa wawili kwenye hospitali ya Kairuki Mikocheni hivyo tumetimiza idadi ya 160 , tunashukuru sana uelewa wa wananchi kuhusu upandikizaji mimba unaendelea kukua siku hadi siku natunatoa elimu,” alisema
Alisema watoto waliozaliwa kwa njia ya upandikizaji mwanzoni kabisa baada ya kuanza kituo hicho wameanza shule na wazazi wao wanatoa ushuhuda namna wanavyofanya vizuri wakiwa shuleni.
“Nimefanyakazi kwenye fani hii kwa Zaidi ya miaka 24 kwa hiyo ninauzoefu mkubwa wa kutosha nina furaha kubwa kuona wanawake ambao awali ilishikana kuwapa huduma hii sasa kutokana na teknojia kukua tunaweza kuwapa huduma hii na wakapata watoto,” alisema Dk Clementina
Alisema huduma hiyo miaka ya nyuma watu walilazimika kuifuata nje ya nchi kwa gharama kubwa lakini kutokana na kuanzishwa kwa KGIVF watu sasa hawana haja ya kupanda ndege kwenda nje ya nchi kwani huduma hizo watazipata hapa nchini.
“Kituo chetu kimepata ithibati ya kimataifa ya ubora kwasababu kinatoa huduma bora ambazo zingeweza kupatikana kwenye mataifa makubwa yaliyoendelea tena kwa gharama kubwa kwenda kule lakini sasa wakija hapa kwetu wanapata huduma kama hizo,” alisema Dk Clementina.
Khadija Seif ambaye ni muuguzi mbobezi wa KGIVF, alisema hivi karibuni alihudhuria kongamano la upandikizaji mimba jijini London Uingereza ambako alijifunza mambo mengi kuhusu teknolojia ya kisasa ya upandikizaji mimba.





