HomeHabariKesi ya Luqman Albusayyid yapangwa kutajwa Oktoba 26

Kesi ya Luqman Albusayyid yapangwa kutajwa Oktoba 26

Upande wa Jamhuri umekamilisha upelelezi wa kesi inayomkabili mfanyabiashara Luqman Issac, maarufu kama Luqman Albusayyid, anayekabiliwa na mashtaka matatu, likiwamo la usafirishaji haramu wa binadamu.

Wakili wa Serikali, Titus Aaron, amedai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Aaron ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo ili upande wa Jamhuri uweze kuandaa nyaraka muhimu kwa ajili ya usikilizwaji, kuzipakia katika mfumo wa mahakama na kumpatia upande wa utetezi.

Hakimu Nyaki amekubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 26, 2026, ambapo mahakama itapanga tarehe ya kumsomea mshtakiwa hoja za awali.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kuwa kati ya Julai 1 na 29, 2026, katika eneo la Magomeni Fundikila, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, alimsafirisha mwanaume mtu mzima kwenda nje ya nchi kwa lengo la unyanyasaji wa kingono.

Katika shtaka la pili, anadaiwa kuwa Agosti 4, 2026, eneo la Msimbazi Center, Mivinjeni, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, alitumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, Nadil Hassan, bila kumjulisha mtoa huduma.

Shtaka la tatu linamhusu mshtakiwa kujipatia kitambulisho cha kupigia kura Machi 2025, katika eneo la Msimbazi, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kwa madai ya kutoa maelezo ya uongo kwa afisa wa usajili kwamba alikuwa raia wa Tanzania, akijua kuwa si kweli.

Mshtakiwa anaendelea kubaki mahabusu kwa kuwa shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu linalomkabili halina dhamana.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments