Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewaonya wakulima na mamlaka za Serikali za mitaa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi, zikiwemo mafuriko, mmomonyoko wa udongo na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na usafirishaji.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, amesema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa kadhaa nchini kuanzia mwishoni mwa Oktoba hadi wiki ya kwanza ya Novemba.
Amesema mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Songwe, Iringa, Njombe na Mbeya inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani kuanzia wiki ya nne ya Oktoba hadi wiki ya kwanza ya Novemba. Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma nayo inatarajiwa kupata mvua hizo kuanzia wiki ya mwisho ya Oktoba.
Katika sekta ya kilimo, Chang’a amesema unyevu mwingi kupita kiasi kwenye udongo na mafuriko vinaweza kuathiri ukuaji wa mazao na kuharibu miundombinu ya kilimo. Pia, hali hiyo inaweza kuongeza magonjwa ya mazao yanayosababishwa na fangasi, bakteria na virusi.
Amesema ingawa shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama kawaida katika baadhi ya maeneo, wakulima wanapaswa kuzingatia taarifa za hali ya hewa na kuchukua hatua zinazofaa kulingana na mazingira yao.
Katika sekta ya usafirishaji, TMA imeonya kuwa mvua kubwa zinaweza kuharibu barabara na miundombinu ya reli za MGR na SGR, na hivyo kuvuruga huduma za usafirishaji.
“Mmomonyoko wa udongo, mafuriko, kuporomoka kwa kingo na kuharibika kwa madaraja kunaweza kuathiri usafiri na kusababisha ajali,” amesema.
Aidha, Chang’a amesema mvua kubwa zinaweza kuathiri shughuli za kiuchumi, hususan bandarini, kwa kuchelewesha upakiaji na upakuaji wa mizigo, hasa shehena zinazohitaji kulindwa dhidi ya unyevu.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka za Serikali za mitaa zimeshauriwa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji ili kupunguza athari za mafuriko na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatua za kuchukua wakati wa mvua kubwa.
TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kuendelea katika kipindi cha msimu wa mvua hadi Aprili na Mei mwaka 2027.
Katika hatua nyingine, Chang’a amesema mifumo ya hali ya hewa inaonesha El Niño ikiendelea kuimarika, huku baadhi ya maeneo nchini yakianza kupata mvua zinazohusishwa na hali hiyo. Amesisitiza umuhimu wa kufuatilia taarifa na tahadhari rasmi za hali ya hewa.




