HomeMichezoPSSSF yatwaa medali mbili Waajiri Health Bonanza

PSSSF yatwaa medali mbili Waajiri Health Bonanza

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetwaa medali mbili katika Bonanza la Tano la Afya la Waajiri, maarufu kama Waajiri Health Bonanza, lililofanyika Oktoba 24, 2026, katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, eneo la Mlimani.

Medali hizo zimepatikana katika mbio za kukimbia huku washiriki wakiwa wamebeba glasi ya maji, kwa wanawake na wanaume. Washindi wamekabidhiwa tuzo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Dk. Evelin Munisi, aliyekuwa mgeni rasmi katika bonanza hilo.

Bonanza hilo lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) linalenga kuhamasisha wafanyakazi kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao, kuongeza tija kazini na kukuza uhusiano kati ya waajiri na taasisi mbalimbali kupitia michezo na burudani.

Akizungumza katika banda la PSSSF, Meneja wa Mfuko Kanda ya Ilala, Amina Kassim, amesema ushiriki wa taasisi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano na wadau, pamoja na kutoa elimu kuhusu huduma za hifadhi ya jamii na mafao yanayotolewa na Mfuko.

“Tuna furaha kuungana na wadau wetu katika bonanza hili. Tunatoa elimu kuhusu huduma zetu, hususan mafao yanayotolewa na Mfuko, chini ya kaulimbiu yetu ya ‘Tunalipa Jana’, ambayo imeufanya Mfuko kwenda hatua ya ziada katika ulipaji wa mafao,” amesema Kassim.

Awali, Dk. Munisi alizindua bonanza hilo kwa kupiga mpira kabla ya kutembelea mabanda ya maonesho, likiwamo la PSSSF, ambako alipokelewa na Kassim.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments