MOTISHA kwa walimu na wanafunzi, pamoja na elimu ya stadi za maisha, zimetajwa kuwa miongoni mwa mikakati inayochangia ufaulu na kuwaandaa wahitimu kujitegemea baada ya kumaliza masomo katika shule za MHL.
Mkurugenzi Mtendaji wa shule hizo, Annasima Mtembei, amesema hayo katika mahafali ya 26 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari St Matthew’s, iliyopo Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Mtembei amesema MHL ina shule nane, zikiwamo tano za sekondari na tatu zinazotoa elimu ya awali na msingi.
Amesema shule hizo zimeweka mfumo wa motisha kwa walimu wanaofanikisha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani, ambapo mwalimu hupata Sh25,000 kwa kila somo ambalo mwanafunzi wake amepata daraja A na Sh20,000 kwa daraja B.
Kwa upande wa wanafunzi, amesema wanaofanya vizuri au kuonyesha vipaji wakiwa darasa la saba wanaweza kupata nafasi ya kusoma bila ada kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Wanafunzi wanaofanya vizuri kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne pia wanaweza kupata nafasi ya kusoma bure kidato cha tano na sita katika shule hizo.
Aidha, amesema wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja katika shule za MHL hunufaika na punguzo la ada.

Mtembei amesema shule hizo zimeweka televisheni katika madarasa kwa ajili ya kusaidia ufundishaji na ujifunzaji, huku wanafunzi wakitumia pia kompyuta za mkononi aina ya tableti.
Ameongeza kuwa, mbali na masomo ya darasani, wanafunzi hufundishwa stadi za maisha, ujasiriamali na nidhamu ya matumizi ya fedha ili kuwawezesha kujiajiri na kujiongezea kipato wanapomaliza masomo.
Amesema shule hizo zimejikita katika misingi mitatu ya elimu, malezi na nidhamu, akiwashukuru wazazi na walezi kwa kuziamini katika kutoa elimu na kuwataka kuendelea kupeleka watoto wao katika shule hizo.
Pia amempongeza wakili Peter Mutembei kwa kutoa mitaji ya fedha kwa wahitimu zaidi ya 100 ili waanzishe biashara baada ya kumaliza masomo na kurejea majumbani.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Jimmy Mkwama, amewataka wahitimu kuendeleza nidhamu waliyojifunza shuleni na kuepuka makundi yanayoweza kuwaingiza katika vitendo visivyofaa kwa jamii.
Mkwama ameipongeza shule hiyo kwa kutoa elimu inayovuka mipaka ya darasani, akisema stadi hizo zinaweza kuwasaidia vijana kujiajiri na kuongeza kipato.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Simon Mlagila, amesema shule hiyo inafundisha michepuo mbalimbali pamoja na lugha za Kichina na Kifaransa, ikiwa na walimu wa lugha hizo.
Risala ya wahitimu iliyosomwa na Godfrey Altwa imeishukuru shule kwa malezi waliyopata na kuiomba Serikali kuzingatia shule binafsi katika utoaji wa motisha za vitabu zinazotolewa kwa shule za Serikali.
Wanafunzi zaidi ya 100 wanatarajiwa kuhitimu kidato cha nne katika shule hiyo mwaka huu.





