HomeAfyaUganda yaunga mkono ajenda ya Samia ya Afya ya Uzazi, yapambana na...

Uganda yaunga mkono ajenda ya Samia ya Afya ya Uzazi, yapambana na malaria

Serikali ya Uganda imeipongeza Tanzania kwa juhudi za kuimarisha afya ya uzazi, mama na mtoto, huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika mapambano dhidi ya malaria na magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi wa Afya wa Uganda anayeshughulikia Huduma za Jumla, Anifa Kawooya Bangirana, alipokutana na ujumbe wa Serikali ya Tanzania jijini Kampala, Oktoba 22, 2026, kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kuhusu mapambano dhidi ya malaria.

Bangirana amesema udhibiti wa malaria ni muhimu katika kulinda afya ya mama na mtoto, kwa kuwa ugonjwa huo unaweza kusababisha madhara kwa wajawazito na watoto, yakiwemo matatizo ya kiafya na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Amesema Uganda inalenga kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030 kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Malaria na Mpango wa Kutokomeza Malaria Busoga (BMEP), unaohusisha Serikali, wadau na jamii katika hatua za kinga, upimaji na matibabu.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria vya Malaria Uganda wa mwaka 2024/2025, asilimia 73 ya wanawake waliokuwa wamejifungua ndani ya miaka miwili kabla ya utafiti walipata angalau dozi tatu za dawa za kinga dhidi ya malaria wakati wa ujauzito, ikilinganishwa na asilimia 41 mwaka 2018/2019.

Hata hivyo, utafiti huo umebaini kuwa kiwango cha maambukizi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59 kiliongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2018/2019 hadi asilimia 13 mwaka 2024/2025, hali inayoonyesha umuhimu wa kuimarisha hatua za kudhibiti ugonjwa huo.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Tanzania, Dk. Sunday Dominico, ambaye ni Naibu Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameweka ajenda ya kufikia malengo matatu ya sifuri ifikapo mwaka 2030.

Amesema malengo hayo ni kutokomeza kujifungulia nyumbani, vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, pamoja na watoto wasiopata chanjo.

Dk. Dominico amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya malaria ni sehemu muhimu ya kufanikisha malengo hayo na kulinda afya ya mama na mtoto barani Afrika.

Naye Dk. Specioza Wandira Kazibwe, Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke wa Uganda mstaafu na Mshauri Mwandamizi wa Rais wa nchi hiyo kuhusu Idadi ya Watu na Afya, amesema majaribio ya awali ya programu ya Busoga yameonyesha matokeo yanayotoa matumaini katika kudhibiti malaria.

Amesema takwimu za majaribio hayo zinaonyesha kupungua kwa msongamano wa mbu aina ya Anopheles kwa asilimia 88.7, huku kiwango cha vipimo vya malaria vilivyokuwa na majibu chanya katika kituo maalumu cha afya kikishuka kutoka takribani asilimia 90.3 hadi asilimia 9.7.

Kazibwe ameikaribisha Tanzania na wadau wengine kutembelea Busoga kujifunza mbinu zinazotumika katika programu hiyo, ikiwemo ushiriki wa jamii katika kuzuia maambukizi, kufuatilia hali ya malaria na kuimarisha upatikanaji wa vipimo na matibabu.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Dk. Dominico na kuambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Meja Jenerali Marco Gaguti, umetembelea maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Iganga, Mkoa wa Busoga, kujifunza namna jamii inavyoshiriki katika utekelezaji wa programu hiyo.

Ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Uganda na kutathmini mbinu zinazoweza kutumiwa kuboresha afua za kinga na udhibiti wa malaria.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments