Benki ya CRDB imeitangaza Tanzania kama kivutio cha uwekezaji katika Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyohitimishwa wiki iliyopita jijini Bangkok, Thailand.
Kupitia jukwaa la CRDB Bank Africa Investor Forum, lililoandaliwa kwa ushirikiano na Invest Africa, Benki hiyo imewakutanisha wawekezaji wa kimataifa na kuangazia fursa za biashara na maendeleo katika masoko inayohudumia ya Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Jukwaa hilo lilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, akiwemo Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar, aliyekuwa Mgeni Rasmi; Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil; na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba.








Miongoni mwa matokeo ya jukwaa hilo ni makubaliano ya dola milioni 75 kutoka FMO ya Uholanzi kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa CRDB kufadhili biashara ndogo na za kati, pamoja na dola milioni 36 kutoka Shelter Afrique Development Bank kusaidia sekta ya makazi na ujenzi. Kati ya fedha hizo, dola milioni 10 zimetengwa kwa ajili ya CRDB Bank DRC.
Benki hiyo pia imepanua ushirikiano na Afreximbank katika biashara, mifumo ya malipo na uwezeshaji wa biashara za wanawake na vijana. Aidha, CRDB imezindua Mwongozo wa Utoaji Taarifa za Athari za Maendeleo Endelevu kwa ushirikiano na J.P. Morgan na Natixis, hatua inayolenga kuimarisha uwazi na kupima mchango wa Benki katika maendeleo.
Huu ni mwaka wa pili kwa CRDB kuandaa jukwaa hilo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na IMF, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuunga mkono diplomasia ya uchumi kwa kuvutia mitaji, kukuza biashara na kuchochea ajira.
















