Tanzania imeshika nafasi ya tano barani Afrika na nafasi ya 80 duniani katika Kielezo cha Chandler cha Utawala Bora Serikalini cha mwaka 2026 (CGGI), baada ya kurekodi maboresho makubwa zaidi katika utendaji wa jumla wa Serikali miongoni mwa nchi 23 za Afrika zilizotathminiwa tangu mwaka 2021.
Kwa mujibu wa Kundi la Chandler la Utawala Bora (CGG), Tanzania imepata ongezeko kubwa la alama katika maeneo ya sheria na sera imara pamoja na taasisi zenye nguvu, huku kiashiria cha ubunifu katika eneo la uongozi na mtazamo wa muda mrefu kikionyesha kupanda kwa nafasi ya nchi hiyo duniani kutoka ya 83 hadi ya 43.
Katika orodha ya Afrika, Tanzania imefuatia Mauritius, Rwanda, Botswana na Morocco zilizoshika nafasi nne za juu, huku Afrika Kusini ikishika nafasi ya sita. Kielezo hicho cha mwaka huu kimepanua wigo wa tathmini hadi nchi 133, zinazowakilisha asilimia 94 ya idadi ya watu duniani, kutoka nchi 120 mwaka 2025.
Mkurugenzi wa Maarifa wa Kundi la Chandler la Utawala Bora, Dinesh Naidu, amesema maendeleo yaliyopatikana katika sheria, sera na taasisi yanaonyesha juhudi za kuimarisha misingi ya Serikali iliyo wazi na yenye ufanisi. Amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha mafanikio hayo yanachangia maboresho katika maeneo mengine ya utendaji wa Serikali.
Hata hivyo, Tanzania imekabiliwa na changamoto katika usimamizi wa fedha za umma pamoja na ushawishi na sifa kimataifa, ambako alama zake zilipungua kati ya mwaka 2021 na 2026. Aidha, nafasi yake duniani katika eneo la taasisi zenye nguvu imeshuka kutoka ya 92 hadi ya 100, licha ya ongezeko la alama.
Kwa upande wa Afrika, wastani wa alama umeongezeka katika maeneo sita kati ya saba yaliyopimwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Hata hivyo, nchi 23 kati ya 35 za Afrika zilizotathminiwa bado ziko nje ya nafasi 100 bora duniani, huku hakuna nchi iliyofanikiwa kuingia katika nafasi 50 bora.
Kielezo cha Chandler cha Utawala Bora Serikalini hutumia viashiria 35 vilivyogawanywa katika maeneo makuu saba kutathmini uwezo na ufanisi wa Serikali. Kinalenga kusaidia nchi kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, kufuatilia maendeleo na kujifunza kutoka kwa mifumo ya utawala inayotumiwa na nchi nyingine.




