HomeBiasharaKiwanda cha Simba Beverages chatajwa kuwa mdau wa Bonde la Wami/Ruvu

Kiwanda cha Simba Beverages chatajwa kuwa mdau wa Bonde la Wami/Ruvu

📌 Ni kiwanda cha vinywaji baridi cha Simba beverages Limited kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani;

📌 Asifu uwekezaji mkubwa bilioni 28 wa kiwanda hicho sambamba na asilimia 90 ya ajira za wazawa;

📌 Serikali yasisitiza uzalishaji wa bidhaa bora na salama, matumizi ya malighafi za ndani, uhamishaji wa teknolojia na uongezaji wa ajira kwa Watanzania.

📌 Bonde la Wami/Ruvu lakumbusha viwanda kulipa ada za maji

📌 Ulipaji wa ada za maji kusaidia utekelezaji wa mipango ya bonde

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameipongeza kampuni ya Simba Beverages Limited kwa kuwekeza takribani Sh bilioni 28 katika sekta ya viwanda nchini, akisema uwekezaji huo unachangia uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi, kuongeza ajira na kupanua wigo wa mapato ya Serikali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la viwanda la Zegereni, Kibaha, mkoani Pwani, Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji na kufungua viwanda vipya ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Amesema sekta ya vinywaji baridi ni muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda kutokana na mchango wake katika uzalishaji, ajira na uwekezaji, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi zikiwemo kilimo, usindikaji na usambazaji wa bidhaa. Amewataka wawekezaji kuongeza matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinazingatia sheria, kanuni na viwango vya ubora na usalama.

Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Kanda ya Kibaha, Innocent Paul, amesema Simba Beverages Limited ni miongoni mwa wadau wa bonde hilo, huku akiwapongeza kwa kufungua kiwanda hicho.

Paul amewataka wadau wa bonde hilo, wakiwemo wawekezaji wa viwanda, kulipa kwa wakati ada za matumizi ya maji ili kuiwezesha bodi kutekeleza mipango yake ya kusimamia na kulinda rasilimali za maji. Amesisitiza kuwa ulipaji wa ada hizo kwa wakati ni sehemu ya wajibu wa watumiaji wa maji wanaotumia rasilimali hiyo kwa shughuli za kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Fadhili Nkurlu, amesema idadi ya viwanda mkoani Pwani imeongezeka kutoka 387 katika mwaka 2021/2022 hadi kufikia 768 Septemba 2026. Amesema viwanda hivyo vinajumuisha vikubwa 33, vya kati 33, vidogo 248 na vidogo zaidi 454.

Nkurlu ameongeza kuwa viwanda vikubwa na vya kati 38 vilivyokuwa katika hatua za ujenzi vimekamilika, huku viwanda vingine 99 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na maandalizi. Amesema viwanda 35 vilivyopo katika maeneo ya uwekezaji mkoani humo vimechangia ajira za moja kwa moja 2,357 na ajira nyingine zisizo rasmi 6,062 zinazotokana na shughuli zinazohusiana na viwanda hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika hafla hiyo, kiwanda cha Simba Beverages Limited kinazalisha vinywaji baridi vyenye gesi pamoja na vifungashio vya plastiki. Mitambo yake ina uwezo wa kuzalisha chupa 12,000 za vinywaji kwa saa, huku kampuni ikitarajia kutoa ajira za moja kwa moja 100 na ajira nyingine 200 zisizo za moja kwa moja kadri shughuli zake zitakavyopanuka.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa inatumia zaidi ya asilimia 90 ya malighafi zinazopatikana nchini, hatua inayolenga kuimarisha uzalishaji wa ndani na mnyororo wa thamani. Pia, inalenga kuongeza mauzo hadi Sh bilioni 15.4 ifikapo mwaka 2027 na Sh bilioni 33 ifikapo mwaka 2030.

Uwekezaji huo unaonesha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uzalishaji wa ndani na kuongeza ajira, huku usimamizi endelevu wa rasilimali za maji ukiendelea kuwa muhimu kwa viwanda vinavyotegemea maji katika shughuli zao za uzalishaji.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments