Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Shirika la Bandari Zanzibar, kuanza mapema maandalizi ya vifaa, mifumo na watumishi watakaohitajika katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani ili iweze kuanza kutoa huduma kwa ufanisi mara tu ujenzi utakapokamilika.
Omar ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo ya kimkakati Zanzibar, inayotarajiwa kukamilika Septemba 2028, akisisitiza umuhimu wa taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma kujiandaa sambamba na ujenzi wa miundombinu.
Amesema bandari hiyo inatarajiwa kuwa miundombinu muhimu ya biashara na usafirishaji wa mizigo kutokana na uwezo wake wa kuhudumia meli kubwa, huku ikiimarisha shughuli za forodha na kuongeza mapato ya Serikali kupitia ushuru wa forodha.
“Pamoja na ujenzi wa miundombinu ya bandari, ni muhimu taasisi zote zinazohusika na utoaji wa huduma kuhakikisha zinapanga kwa pamoja mahitaji yao ili kuepusha bandari kukamilika huku vifaa na mifumo muhimu ya uendeshaji ikiwa haijakamilika,” amesema Omar.




Amezitaka TRA na Shirika la Bandari Zanzibar kuoanisha ratiba za utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha vifaa, mifumo na watumishi vinapatikana kwa wakati na huduma zinaanza bila ucheleweshaji usio wa lazima.
Omar amesema ameridhishwa na taarifa ya maendeleo ya mradi inayoonyesha kuwa ujenzi umefikia takribani asilimia 20, hatua inayolingana na matarajio ya utekelezaji kwa kipindi husika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, amesema bandari hiyo ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia kuimarisha biashara na usafirishaji wa mizigo.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni muhimu katika kuhakikisha bandari hiyo inakuwa kitovu cha biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi.
Khamis ameeleza kuwa maandalizi yanahusisha upatikanaji wa maeneo ya kuhifadhi mizigo, vifaa vya ukaguzi wa mizigo, ikiwamo mashine za uchunguzi (scanners), pamoja na mifumo na vifaa vya TRA vitakavyowezesha shughuli za forodha na usafirishaji wa mizigo inayopita bandarini kwenda maeneo mengine (transshipment) kufanyika kwa ufanisi.
Amesema awamu ya kwanza ya bandari hiyo itakapokamilika Septemba 2028, itakuwa na uwezo wa kuhudumia makontena kati ya 250,000 na 300,000 kwa mwaka, pamoja na tani 500,000 hadi milioni moja za mizigo ya kawaida isiyohifadhiwa kwenye makontena.
Ameongeza kuwa uwezo wa bandari hiyo unaweza kuongezwa katika awamu zijazo kwa kupanua maeneo ya kuhifadhi mizigo na miundombinu mingine kulingana na mahitaji ya biashara.
Khamis amesema kukamilika kwa mradi huo, pamoja na maandalizi ya mapema ya taasisi zitakazotoa huduma, kunatarajiwa kuimarisha uwezo wa Zanzibar kuhudumia biashara ya kimataifa, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kufungua fursa mpya za uwekezaji.








