Wake za Askari Mkoa wa Morogoro wameadhimisha sherehe za umoja wao kwa lengo la kuimarisha upendo, mshikamano, kufahamiana na kukuza chama chao cha Umoja wa wawanawake wa askari mkoani humo ambapo Sherehe hizo zimefanyika Novemba 1, 2026 katika Ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe, Manispaa ya Morogoro.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Andrew Kantimbo, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, ACP Samweli Kijanga.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, ACP Kijanga alianza kwa kuwapongeza waandaaji wa sherehe hizo kwa ubunifu na hatua nzuri waliyoifanya ya kuwakutanisha wake za askari katika kuimarisha umoja, upendo na mshikamano.
Aidha, aliwasisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto ndani na nje ya kambi za Polisi, akieleza kuwa watoto wa askari wanapaswa kuwa mfano mzuri katika jamii kwa kuzingatia maadili na nidhamu.




Alieleza kuwa ustawi wa askari wa kiume kazini unaimarika pale wanapotoka katika familia zenye upendo, amani na mshikamano, hali inayochangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika hatua nyingine, alimuelekeza Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Zena, kuhakikisha wake za askari wanapata elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, pamoja na kumuelekeza Mwenyekiti Msaidizi wa TPF Net kuhakikisha mtandao huo unatoa ushirikiano wa kutosha kwa wake za askari ili kuunga mkono jitihada na shughuli wanazoanzisha.
Pia, mgeni rasmi alipokea ombi la kuzungumza na askari wa kiume kwa lengo la kuwaunga mkono wake zao katika kuimarisha umoja na mshikamano.
Katika sherehe hizo, wake za askari waliwasilisha maombi mbalimbali, ikiwemo kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi na askari wa kike, kuelimishwa kwa waume zao ili wasiwazuie kushiriki katika vikao na shughuli mbalimbali zinazowakutanisha, pamoja na kupata elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, malezi bora na nafasi yao kama wake za askari.




Akizungumza katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa Umoja wa wake za askari Wilaya ya Morogoro, Madam Evelin, alipata wasaa wa kuwaelimisha washiriki kuhusu malezi bora ya familia na watoto, akisisitiza umuhimu wa kuwafuatilia na kuwasimamia watoto ili waweze kuwa mfano mzuri katika jamii.
Kwa upande wake, Katibu wa Walimu Mkoa wa Morogoro, bi Tekla Mbiki, alitoa elimu kuhusu kujikwamua kiuchumi, kuweka akiba, kuanzisha vikundi vyenye malengo ya kujenga ustawi wa familia, kujiamini na kujipenda.
Aidha, wawakilishi wa kampuni ya Vodacom na Benki ya NMB walioalikwa katika sherehe hizo walitoa elimu kuhusu fursa za kujikwamua kiuchumi na namna ya kutumia mikopo kwa malengo ya maendeleo.




Naye Kaimu Mwenyekiti wa TPF Net, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP)Matha Mdinka, aliwapongeza wake za askari kwa hatua hiyo kubwa ya kuimarisha umoja wao na kuwaahidi ushirikiano wa kutosha ambapo amewasisitiza umuhimu wa kutoa taarifa na kuzifikisha kwa viongozi ili ziweze kufanyiwa kazi.
Mchungaji Dkt. Rhoda Chamshama kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Mji Mpya, akawakumbusha wanawake hao kuwa vinara wa amani ndani ya ndoa zao kwa kujenga upendo, maelewano na mshikamano, akisisitiza kuwa amani katika familia ni msingi muhimu unaowawezesha waume zao kutekeleza majukumu yao ya kikazi kwa ufanisi zaidi.
Vilevile, aliwahimiza kutunza ndoa zao kwa kuwa ndoa imara ni msingi muhimu wa familia ya Polisi yenye upendo, amani na mshikamano.
Katika kuunga mkono maendeleo ya kikundi hicho, mgeni rasmi aliongoza harambee iliyofanyika kwa kuuza keki zilizoandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo, ambapo jumla ya shilingi 700,000 taslimu zilikusanywa.
Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kikundi hicho kununua viti na kuanza shughuli ya kukodisha viti kama sehemu ya kujikwamua kiuchumi na kuimarisha ustawi wa umoja wao.
Sherehe hizo zimekuwa sehemu muhimu ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa wake za askari Mkoa wa Morogoro, huku zikifungua fursa za kujenga familia imara na kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa manufaa ya wanachama na jamii kwa ujumla.







