HomeHabariAFICD yaongeza kasi ya usafirishaji wa makontena kwa reli

AFICD yaongeza kasi ya usafirishaji wa makontena kwa reli

Usafirishaji wa makontena kwa reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda vituo vya kuhifadhia mizigo nje ya bandari unaendelea kuwa njia muhimu ya kupunguza msongamano wa malori na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo.

Mbali na reli ya kisasa ya SGR, ambayo imeanza pia kusafirisha makontena kwenda Dodoma, African Inland Container Depot (AFICD), iliyopo eneo la TAZARA jijini Dar es Salaam, imeanza kutumia reli kuhamisha makontena kutoka bandarini kwenda kituoni hapo.

Kupitia mfumo huo, makontena yanayowasili bandarini husafirishwa kwa treni hadi AFICD, ambako hupokelewa na baadaye kuchukuliwa na malori kwa ajili ya kupelekwa kwa wateja.

Akizungumza Jumatatu, Novemba 2, 2026, wakati wa ziara iliyowashirikisha wadau wa sekta ya usafirishaji, Meneja wa AFICD, Saeed Bin Argan, amesema kituo hicho kwa sasa kinapokea makontena yasiyopungua 100 kila siku kutoka bandarini kwa kutumia reli.

“Kwa sasa tunahamisha makontena yasiyopungua 100 kwa siku kutoka bandarini kwenda AFICD kwa kutumia reli. Hii inasaidia kupunguza idadi ya malori yanayohitaji kuingia bandarini kuchukua makontena,” amesema Bin Argan.

Amesema kampuni hiyo ina vichwa viwili vya treni vyenye uwezo wa kuvuta mabehewa 60 kwa wakati mmoja, huku ikiwa na mpango wa kuongeza vichwa vingine ili kupanua uwezo wa huduma hiyo.

Hata hivyo, amesema changamoto inayokwamisha matumizi kamili ya miundombinu hiyo ni upatikanaji mdogo wa mizigo, hali inayosababisha uwezo uliopo kutotumika kikamilifu.

Kauli hiyo inaonesha kuwa pamoja na uwepo wa miundombinu na vifaa vya usafirishaji, kuongeza kiwango cha makontena yanayohamishwa kwa reli kunahitaji ushirikiano wa wadau na mipango inayohakikisha mizigo ya kutosha inapatikana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, amesema Bandari ya Dar es Salaam imefanya maboresho katika miundombinu, vifaa na mifumo ya uendeshaji ili kuongeza ufanisi wa shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo.

Maboresho hayo yana umuhimu katika kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo, lakini changamoto ya msongamano wa malori katika barabara zinazozunguka eneo hilo bado imekuwa ikiwaletea usumbufu watumiaji wa barabara.

Julai 11, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati huo, Albert Chalamila, aliagiza wadau wa sekta ya bandari na usafirishaji kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Akizungumzia hali hiyo, Chalamila alisema msongamano wa malori katika barabara za Temeke, Kigamboni na Mandela ulikuwa ukisababisha usumbufu kwa wananchi, wakiwemo wafanyakazi waliochelewa kufika kazini kutokana na foleni.

“Njia ya Temeke, Kigamboni na Mandela hali ni mbaya. Kila unapokwenda unakuta malori yamepaki yakisubiri kwenda bandarini au kutoka. Mjazano wa magari umeibua malalamiko makubwa, watu wanaingia kazini saa tatu, saa nne,” alisema Chalamila.

Kwa kuzingatia changamoto hizo, matumizi ya reli kuhamisha makontena kwenda vituo vya nje ya bandari yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kupunguza idadi ya malori yanayoingia bandarini na muda wa kusubiri huduma.

Hata hivyo, mafanikio ya mfumo huo yatategemea uwezo wa kuongeza kiwango cha mizigo inayosafirishwa kwa reli, pamoja na uratibu mzuri kati ya bandari, waendeshaji wa reli na vituo vya kuhifadhia makontena.

Kwa kuwa malori bado yanahitajika kusafirisha makontena kutoka vituoni kwenda kwa wateja, mfumo huo hauondoi kabisa matumizi ya barabara, bali unaweza kupunguza safari za malori kuingia moja kwa moja bandarini na hivyo kupunguza shinikizo la magari katika maeneo yanayozunguka bandari.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments