Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka lengo la kukusanya Sh trilioni 42 katika mwaka wa fedha 2025/26, kutoka Sh trilioni 37 zilizokusanywa mwaka uliopita, huku ikisisitiza umuhimu wa kukuza viwanda na biashara ili kuongeza wigo wa mapato ya Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Paul John Walalaze, amesema ukuaji wa viwanda na biashara ni miongoni mwa vichocheo muhimu vya kuongeza mapato ya Serikali na kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dodoma Novemba 2, 2026, katika maonesho yanayoelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, Walalaze amesema TRA itaendelea kushirikiana na wenye viwanda pamoja na wafanyabiashara kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha shughuli zao kukua.
Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali yanayolenga kurahisisha ufanyaji biashara, kuimarisha sekta ya viwanda na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mitaji na fursa za kupanua shughuli zao.




Ameeleza kuwa mwaka wa fedha 2025/26 ni wa kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayoweka msisitizo katika maendeleo ya viwanda na sekta binafsi kama nguzo za kufikia malengo ya uchumi wa taifa.
Walalaze amesema kuimarika kwa mazingira ya biashara kutasaidia kuongeza shughuli za uzalishaji na biashara, kupanua wigo wa walipa kodi na kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinaendana na azma ya Tanzania kujenga uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Katika hatua nyingine, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa risiti za mauzo kwa wateja, huku wananchi wakihimizwa kudai risiti kila wanaponunua bidhaa au kupata huduma.
Amesema matumizi sahihi ya risiti ni muhimu katika utambuzi na usimamizi wa kodi, na kwamba mapato yanayokusanywa na Serikali husaidia kugharamia huduma za kijamii na kutekeleza miradi ya maendeleo.zima.







