HomeHabariTanzania yalenga megawati 70 za umeme ifikapo 2050

Tanzania yalenga megawati 70 za umeme ifikapo 2050

Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka gigawati 4.6 za sasa hadi gigawati 70 ifikapo mwaka 2050, huku nishati ya jua ikitarajiwa kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya kufanikisha azma hiyo.

Katika kufikia lengo hilo, Serikali imeeleza maeneo yanayohitaji ushirikiano wa kimataifa katika uwekezaji, teknolojia na utaalamu wa nishati ya jua, ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Mwakilishi wa Tanzania katika Muungano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA), Emilian Nyanda, kutoka Wizara ya Nishati, amesema hayo Novemba 3, 2026, wakati wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa muungano huo unaofanyika nchini India na kushirikisha nchi wanachama pamoja na washirika wa maendeleo zaidi ya 125.

Amesema Serikali imeweka mkazo katika kuendeleza nishati jadidifu, hususan nishati ya jua, ili kuongeza uzalishaji wa umeme, kupanua huduma katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya taifa na kuchangia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Nyanda, Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi gigawati nane ifikapo mwaka 2030, kabla ya kufikia gigawati 70 mwaka 2050, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema tayari nchi imeanza kutekeleza miradi ya uzalishaji wa umeme wa jua, ukiwemo mradi wa Kishapu mkoani Shinyanga wenye uwezo wa jumla wa megawati 150.

Katika mradi huo, awamu ya kwanza yenye uwezo wa megawati 50 imekamilika, huku awamu ya pili ya megawati 100 ikiendelea kutekelezwa.

Ameongeza kuwa kwa sasa megawati 100 za umeme wa jua zinaingizwa katika gridi ya taifa, huku Serikali ikilenga kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kwa megawati 1,000 ifikapo mwaka 2035 kupitia uwekezaji wa sekta ya umma na binafsi.

Katika kuimarisha uwekezaji, Nyanda amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea kutambua na kutenga maeneo yanayofaa kwa miradi ya nishati ya jua, kufanya tafiti za upembuzi yakinifu na tathmini za athari kwa mazingira.

Amesema hatua hizo zinalenga kupunguza gharama za awali za uwekezaji na kuweka mazingira yatakayovutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo.

Mbali na kuingiza umeme kwenye gridi ya taifa, amesema Tanzania inaendelea kutumia teknolojia ya nishati ya jua kufikisha huduma katika maeneo ya mbali ambayo hayajafikiwa na gridi, yakiwemo visiwa vilivyopo katika Maziwa Makuu na Bahari ya Hindi.

Nishati hiyo pia inatumika katika shughuli za uzalishaji mali, zikiwemo kilimo, umwagiliaji, usindikaji wa mazao, uvuvi, ufugaji na usambazaji wa maji.

Kuhusu maendeleo ya utaalamu wa ndani, Nyanda amepongeza ushirikiano kati ya Tanzania na ISA uliowezesha kuanzishwa kwa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Teknolojia ya Nishati ya Jua (STAR-C) katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Amesema kituo hicho kinatoa mafunzo kwa wataalamu wa ndani, huku Watanzania wengine wakinufaika na mafunzo ya kitaalamu katika taasisi mbalimbali za kimataifa.

Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa ISA, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuvutia mitaji, teknolojia na utaalamu utakaoharakisha utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu.

Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa India anayeshughulikia masuala ya Nishati Jadidifu, Pralhad Joshi, ambaye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha nishati ya jua inapatikana kwa gharama nafuu.

Joshi pia ametoa wito wa kuongeza uwekezaji katika nishati safi, hususan katika nchi zinazoendelea, ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments