HomeBiasharaWaendesha bodaboda wajengewa uwezo wa kuokoa maisha

Waendesha bodaboda wajengewa uwezo wa kuokoa maisha

Waendesha pikipiki 1,624 jijini Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani na huduma ya kwanza kupitia ushirikiano kati ya Kampuni ya Tanzania Breweries PLC (TBL) na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), hatua inayolenga kupunguza ajali na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na dharura.

Idadi hiyo imevuka lengo la awali la kuwafikia waendesha pikipiki 1,600, sawa na utekelezaji wa asilimia 102, kupitia mafunzo yaliyofanyika katika wilaya zote tano za Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yamejikita katika uendeshaji wa tahadhari, sheria na kanuni za usalama barabarani, matumizi sahihi ya helmeti, hatua za kuchukua wakati wa dharura na kufanya maamuzi salama wanapotumia barabara.

Ushirikiano huo ulioanza mwaka 2024 unatambua nafasi ya waendesha pikipiki za biashara katika usafiri na shughuli za kiuchumi, lakini pia uwezekano wao wa kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika maeneo ya ajali na kutoa msaada wa awali.

Akizungumzia mpango huo, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Uhusiano wa Kampuni wa TBL, Neema Temba, amesema usalama barabarani unahusu kulinda maisha, familia na vyanzo vya kipato vya wananchi.

Amesema mafunzo hayo yanawapatia waendesha pikipiki maarifa na stadi za kufanya maamuzi salama barabarani, huku mwitikio wao na kuvuka lengo la washiriki vikionyesha umuhimu wa programu hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, Lucia Pande, amesema usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja na kwamba mafunzo ya huduma ya kwanza yanaweza kuongeza uwezo wa jamii kutoa msaada wa haraka wakati wa ajali.

Amesema ushirikiano huo unaimarisha uelewa wa watumiaji wa barabara na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na dharura.

Katika kuendeleza ajenda ya usalama, TBL pia inahimiza matumizi ya pombe kwa uwajibikaji, ikisisitiza kuwa unywaji wa pombe na uendeshaji wa pikipiki haviendani.

Kampuni hiyo imesema itaendelea kushirikiana na wadau kupanua elimu ya usalama barabarani na huduma ya kwanza ili kuwafikia watumiaji wengi zaidi wa barabara nchini.

Mafanikio ya mafunzo kwa wilaya

WilayaLengoWaliofunzwaMafanikio
Kinondoni345347101%
Kigamboni235245104%
Ilala335335100%
Temeke378384102%
Ubungo307313102%
Jumla1,6001,624102%
RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments