Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kwenda sambamba na kuwawezesha vijana kupata ujuzi na ajira za kijani zitakazochochea maendeleo ya uchumi na kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Akizungumza katika Mkutano wa 31 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaofanyika Antalya, Uturuki, Rais Samia amesema Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya miaka 25 ijayo imeweka kipaumbele katika ubunifu, ujenzi wa viwanda na mageuzi endelevu ya uchumi, yanayohitaji vijana kuandaliwa kushiriki katika fursa mpya za uchumi wa kijani.

Amesema fursa hizo zinapatikana katika sekta za nishati jadidifu, kilimo endelevu na viwanda rafiki kwa mazingira, hivyo ni muhimu kuwekeza katika teknolojia na kuwajengea vijana uwezo ili wawe sehemu ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania inalenga kuhakikisha hatua za tabianchi zinatoa fursa za maendeleo kwa vizazi vijavyo, huku akihimiza ushirikiano wa kimataifa katika upatikanaji wa fedha, teknolojia na kujenga uwezo wa kutekeleza mipango hiyo.





