HomeBiasharaCarbon Bridge kuvutiwa na fursa za biashara ya kaboni Tanzania

Carbon Bridge kuvutiwa na fursa za biashara ya kaboni Tanzania

Kampuni ya Carbon Bridge imeonesha nia ya kuongeza uwekezaji katika biashara ya kaboni nchini Tanzania, ikivutiwa na fursa zilizopo katika sekta za nishati safi, misitu, kilimo na usimamizi wa taka, zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Nia hiyo imeelezwa katika mazungumzo kati ya kampuni hiyo na wataalamu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaoendelea jijini Antalya, Uturuki.

Katika majadiliano hayo, Carbon Bridge imeeleza kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini, uwepo wa miradi yenye uwezo wa kuzalisha viwango vikubwa vya mikopo ya kaboni (carbon credits), pamoja na mfumo wa uratibu na usimamizi wa biashara hiyo unaosimamiwa na Serikali kupitia NCMC.

Kampuni hiyo tayari imewekeza katika biashara ya kaboni kupitia miradi inayohusisha nishati safi ya kupikia na matumizi ya majiko yaliyoboreshwa, huku ikionesha nia ya kutumia fursa nyingine zilizopo katika sekta hiyo nchini.

Kwa upande wake, wataalamu wa NCMC wameeleza utayari wa kutoa ushirikiano wa kitaalamu na kuratibu hatua mbalimbali za uwekezaji na utekelezaji wa miradi hiyo, kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali inayosimamia biashara ya kaboni nchini.

Mazungumzo hayo pia yamelenga kubainisha maeneo ya kimkakati ya uwekezaji, kuimarisha uratibu kati ya Serikali na wawekezaji, pamoja na kuhakikisha miradi ya kaboni inazingatia viwango vya uadilifu wa kaboni ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Kwa sasa, Tanzania inaendelea kufungua fursa za uwekezaji katika biashara ya kaboni kupitia sekta za misitu, kilimo, nishati, maji na usimamizi wa taka. Sekta hizo zina uwezo wa kuvutia mitaji, kuzalisha mikopo ya kaboni, kuongeza kipato cha jamii na kuchochea maendeleo endelevu.

Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) ni taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yenye jukumu la kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa biashara ya kaboni nchini.

Majukumu mengine ya kituo hicho ni kutoa ushauri wa kitaalamu, kufuatilia usajili na utekelezaji wa miradi, pamoja na kuhakikisha taarifa za miradi ya biashara ya kaboni zinazingatia mifumo na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Ushiriki wa NCMC katika mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama eneo lenye fursa za uwekezaji wa biashara ya kaboni, kuimarisha ushirikiano na wawekezaji wa kimataifa na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa tija na kuleta manufaa kwa taifa.

Katika mkutano huo, NCMC iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji, Usajili na Utoaji Taarifa za Miradi, Dkt. Deo Shirima; Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Mazingira, Ushauri na Utafiti, Dkt. Paul Lyimo; Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Risper Koyi; na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ibrahim Hamidu.

Kwa upande wa Carbon Bridge, washiriki walikuwa Afisa Mtendaji Mkuu, Marion Verles; Afisa Mkuu wa Masuala ya Kaboni, Donee Alexander; na Mkurugenzi wa Sera na Maendeleo ya Biashara, Fabio Marque.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments