HomeBiasharaExim Bank ya Uturuki kujadili ufadhili wa SGR

Exim Bank ya Uturuki kujadili ufadhili wa SGR

Serikali ya Tanzania iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Benki ya Exim ya Uturuki kutafuta ufadhili wa dola za Marekani milioni 280 (takribani Sh. bilioni 728, kutegemea kiwango cha ubadilishaji) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vipande vya tatu na nne vya Reli ya Kisasa (SGR), vyenye urefu wa zaidi ya kilomita 700.

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Antalya, Uturuki, pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), kati ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, na ujumbe wa Benki ya Exim ya Uturuki ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Ali Guney.

Balozi Omar amesema mradi huo una thamani ya jumla ya dola za Marekani bilioni 1.6, ambapo tayari Serikali imefanikiwa kupata dola bilioni 1.32, huku kiasi cha dola milioni 280 kikihitajika kukamilisha fedha za ujenzi wa vipande hivyo viwili.

Amesema SGR ni mradi mkubwa wa kimkakati wenye mtandao wa zaidi ya kilomita 2,000, unaolenga kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na mikoa ya magharibi, ikiwemo Mwanza na Kigoma, pamoja na nchi jirani za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ameeleza kuwa mradi huo umegawanywa katika sehemu sita zinazojulikana kama loti, huku loti mbili za kwanza zinazounganisha Dar es Salaam na Dodoma zikiwa zimekamilika, zimeanza kutoa huduma na kupokelewa vizuri na wananchi.

Amesema tofauti na miradi mingi ya reli katika ukanda wa Afrika inayotumia nishati ya dizeli, SGR ya Tanzania inatumia umeme, hatua inayoiweka katika mwelekeo wa usafiri wenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira na ajenda ya mpito wa nishati safi inayojadiliwa katika COP31.

Kwa upande wake, Guney amesema benki hiyo inatambua umuhimu wa mradi huo katika maendeleo ya Tanzania na nchi jirani, akieleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo inatarajiwa kukutana mwezi huu kujadili maombi ya ufadhili wa dola milioni 280.

Amesema mbali na mradi wa reli, benki hiyo pia inachunguza maeneo mengine ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na Uturuki, ikiwemo ufadhili wa miradi ya miundombinu ya baadaye kama barabara na madaraja.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kupanua wigo wa uwekezaji na biashara kati ya mataifa hayo mawili, sambamba na malengo yaliyowekwa na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoÄŸan, ya kukuza biashara baina ya nchi hizo na kufikia thamani ya angalau dola za Marekani bilioni moja.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments