Tanzania imeeleza utayari wa kuimarisha tafiti za kisayansi kuhusu vyakula vya asili ili kubaini mchango wake katika kuboresha lishe na kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, amesema hayo wakati akifungua kongamano la kisayansi la Mpango wa Lishe Duniani (World Diet Initiative), lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili za lishe, ambazo ni udumavu na upungufu wa virutubisho muhimu kwa upande mmoja, huku uzito uliopitiliza, unene uliokithiri na magonjwa yanayohusishwa na mtindo wa maisha vikiongezeka kwa upande mwingine.
Amesisitiza kuwa hali hiyo inahitaji kuimarisha mikakati ya kukabiliana na chanzo cha matatizo hayo, ikiwemo ulaji usiofaa na mabadiliko ya mazingira ya upatikanaji wa chakula.




Hata hivyo, Profesa Sunguya amesisitiza kuwa vyakula vya asili havipaswi kutangazwa kuwa kinga au tiba ya magonjwa bila ushahidi wa kutosha wa kisayansi, hivyo kutaka kufanyika kwa tafiti kuhusu virutubisho, namna ya kuandaa na uwiano sahihi wa mlo.
Kongamano hilo limewakutanisha wanasayansi, watunga sera na wataalamu wa afya ya jamii kutoka zaidi ya nchi 16, zikiwemo Uholanzi, Marekani, Brazil, India na Romania, kwa lengo la kujadili mchango wa mifumo ya vyakula vya asili katika afya ya jamii.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Sabina Mugusi, amesema ukuaji wa miji, utandawazi na ongezeko la vyakula vilivyosindikwa viwandani vinabadilisha kwa kasi mfumo wa ulaji nchini.
Amesema watafiti wanapaswa kuhakikisha matokeo ya tafiti zao yanageuzwa kuwa suluhu zinazotekelezeka, zinazozingatia tamaduni za jamii na uwezo wa kiuchumi wa wananchi.






Ameongeza kuwa kongamano hilo linalenga kuweka ajenda ya pamoja ya utafiti wa kimataifa ili kuhifadhi maarifa na mapishi ya vyakula vya asili yanayopotea na kuimarisha mikakati ya lishe endelevu.
Akieleza matokeo ya tafiti, Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha KCMC, Dk. Godfrey Temba, amesema utafiti wa awali wa miaka saba uliofanyika mkoani Kilimanjaro umebaini uwepo wa virutubisho na vimelea hai vyenye manufaa katika baadhi ya vyakula vya asili.
Ametaja vyakula hivyo kuwa ni kiburu, kinachoandaliwa kwa mchanganyiko wa maharage na ndizi, mazao ya mizizi pamoja na mbege, kinywaji cha asili kinachotengenezwa kwa kuchachusha ulezi na ndizi.
Amesema matokeo hayo yanaonyesha umuhimu wa kuendelea kuchunguza mchango wa vyakula hivyo katika kuimarisha afya na kupunguza vihatarishi vya magonjwa sugu.








