HomeBiasharaHomera atafuta fedha za kuendeleza nishati safi

Homera atafuta fedha za kuendeleza nishati safi

📌Azungumza na SEforALL na UpEnergy kujadili fursa za kuimarisha matumizi ha nishati safi ya kupikia

Antalya, Uturuki – Novemba 13, 2026

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Homera, ameshiriki mijadala ya ngazi ya juu kuhusu mpito wa nishati safi, usalama wa nishati na upatikanaji wa umeme, sambamba na kufanya mikutano ya uwili na wadau wa kimataifa wa maendeleo na uwekezaji, pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaoendelea jijini Antalya, Uturuki.

Katika Mjadala wa Ngazi ya Juu kuhusu Mpito wa Nishati Safi na Usambazaji wa Umeme, uliopewa jina la “35 by 35: Powering the Future” na kufanyika Novemba 11, 2026, Waziri Homera, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaunga mkono mpango huo wa kimataifa unaolenga kuongeza mchango wa umeme katika matumizi ya nishati duniani kufikia asilimia 35 ifikapo mwaka 2035.

“Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha sekta ya umeme, ambapo uwezo wetu wa uzalishaji umefikia zaidi ya megawati 4,600, huku vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vikiwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati, tunalenga kuongeza kiwango cha uunganishaji wa umeme kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uwezo wa uzalishaji wa umeme kufikia asilimia 75,” amesema Waziri Homera.

Aidha, Waziri Homera ameshiriki Mkutano wa Ngazi ya Juu uliojadili mada ya “Powering the Future: Grids for Energy Security and Prosperity”, uliojikita katika Mpango wa Kimataifa wa Kuharakisha Maendeleo ya Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (Global Grid Accelerator). Mpango huo unalenga kuimarisha miundombinu ya gridi za umeme ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha usalama wa nishati na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Katika mikutano ya uwili, Waziri Homera amekutana na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Nishati Endelevu kwa Wote, ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Sustainable Energy for All (SEforALL) na Mwenyekiti Mwenza wa UN-Energy, Bi. Damilola Ogunbiyi.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini, hususan katika taasisi za umma zikiwemo shule na vituo vya afya, pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa fedha za uwekezaji katika eneo hilo.

Bi. Ogunbiyi ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake katika kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia barani Afrika na kueleza utayari wa SEforALL kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuharakisha utekelezaji wa mipango hiyo.

Vilevile, Waziri Homera amekutana na uongozi wa kampuni ya UpEnergy, ambapo wamejadiliana kuhusu fursa za kutumia mifumo ya biashara ya hewa ukaa (Carbon Credits) kuvutia uwekezaji na kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, hususan katika taasisi zikiwemo shule na vituo vya afya.

“Biashara ya hewa ukaa ni miongoni mwa fursa zinazoweza kutumika kuvutia uwekezaji na kupunguza gharama za teknolojia za nishati safi ya kupikia, hivyo kusaidia kuongeza kasi ya matumizi ya nishati hiyo katika taasisi na kwa wananchi,” amesema Waziri Homera.

Ushiriki wa Waziri Homera katika mijadala hiyo ya kimataifa na mikutano ya uwili unaonesha jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuhamasisha rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya nishati.

Hatua hizo pia zinaunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments