Upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika kwa wananchi unatarajiwa kuimarika kupitia mikakati ya kupunguza upotevu wa maji na kuboresha miundombinu, iliyojadiliwa na viongozi wa EWURA na DAWASA.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Salum Mnuna, amekutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire, Novemba 19, 2026, kujadili utekelezaji wa mikakati hiyo.
Katika kikao hicho, Mnuna amesisitiza umuhimu wa DAWASA kuimarisha hatua za kupunguza upotevu wa maji na kuboresha miundombinu ili kuongeza ufanisi wa uendeshaji, upatikanaji na uhakika wa huduma kwa wananchi.
Amesema wamejadili pia matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji, uchakataji na uwasilishaji wa taarifa, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa mamlaka hiyo.
Ameeleza kuwa EWURA inaendelea kusimamia utendaji wa mamlaka za maji, ikiwamo DAWASA, kwa kuhakikisha zinazingatia viwango vya utoaji huduma ili wananchi wapate huduma bora, endelevu na kwa gharama stahiki.




