Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepanga kukusanya Shilingi Bilioni 25 kupitia kongamano la hisani la JKCI-HTAF Prestige Gala Dinner 2026 litakalofanyika Desemba 4, 2026 katika hoteli ya Malaika Beach Resort, Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 10 zitatumika moja kwa moja kugharamia matibabu ya watoto 1,000 wanaosubiri upasuaji.
Dkt. Kisenge amesema licha ya mafanikio makubwa katika miaka 11 tangu JKCI ianzishwe rasmi mwaka 2015 kutoka kitengo cha moyo cha Hospitali ya Taifa Muhimbili hadi kuwa Kituo cha Rufaa cha Afrika, mahitaji bado ni makubwa.
“Zaidi ya watoto 16,000 huzaliwa nchini kila mwaka wakiwa na matatizo ya moyo. Kati yao, takribani 4,000 wanahitaji upasuaji wa haraka. Hivi sasa, zaidi ya watoto 1,500 wako kwenye orodha ya kusubiri upasuaji katika taasisi yetu,” alisema Dkt. Kisenge.




Ameongeza kuwa gharama ya matibabu ya mtoto mmoja ni kati ya Shilingi Milioni 8 hadi 16, ambapo Serikali huchangia asilimia 70 na mzazi huchangia asilimia 30. Changamoto kubwa ni wazazi wengi kushindwa kumudu hata hiyo asilimia 30.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu kuanzishwa kwake, JKCI imeokoa maisha ya zaidi ya watu milioni moja na kuiokoa Serikali zaidi ya Shilingi Bilioni 172 ambazo zingetumika kutibu wagonjwa nje ya nchi. Katika kipindi cha miaka 10 pekee, taasisi hiyo imewahudumia wagonjwa 745,837 wakiwemo watoto 71,184.
Ili kukabiliana na changamoto ya fedha, JKCI ilianzisha mwaka 2023 taasisi ya hisani ya Heart Team Africa Foundation (HTAF).
Gala Dinner ya mwaka huu itakayobeba kaulimbiu ya “Okoa Moyo wa Mtoto, Okoa Taifa” inalenga pia ujenzi wa nyumba ya mapumziko kwa watoto na familia zao.
Katika tukio hilo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dk. Kisenge ametoa wito kwa sekta binafsi, benki, makampuni ya madini na mawasiliano, na Watanzania wote kuchangia.
“Shilingi Milioni 10 zinatibu mtoto mmoja. Shilingi Bilioni 1 zinatibu watoto 100. Tukifikia lengo la bilioni 10, tutaweza kuwatibu watoto 1,000 na kupunguza kwa kiasi kikubwa orodha ya kusubiri,” alisisitiza.








