Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema uwekezaji katika michezo unahitaji ushiriki wa sekta zote ili kukuza vipaji na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Nanauka, ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Mjini, ameyasema hayo wakati wa mechi ya kirafiki kati ya timu ya kombaini ya wachezaji kutoka CRDB Nanauka Cup na timu ya Benki ya CRDB, mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Ameipongeza benki hiyo kwa kuwekeza katika michezo ya aina mbalimbali nchini, akisema ushiriki wa taasisi za kifedha na wadau wengine unasaidia vijana kupata fursa za kuonesha vipaji vyao na kujipatia kipato.
Amesema mechi hiyo iliyohudhuriwa na makocha wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wadau wengine wa michezo imewapa vijana nafasi ya kuonesha uwezo wao mbele ya watu wanaoweza kuwasaidia kupiga hatua katika taaluma ya soka.
“Mechi hii imehudhuriwa na makocha wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wadau wengine wa michezo. Ni sehemu nzuri kwa vijana wetu kujiuza. Michezo ni moja ya nguzo muhimu za ajira kwa vijana. Tuna vipaji vingi sana nchini. Nawashukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha michezo nchini,” amesema.




Mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, imemalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Wafanyakazi wa Benki ya CRDB, Timothy Fasha, amesema udhamini wa michezo unaolenga kuwapa vijana fursa ya kutumia vipaji vyao kujenga maisha na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesema benki hiyo inaamini uwekezaji kwa vijana ni sehemu muhimu ya kujenga jamii inayoweza kujitegemea, huku michezo ikiwa jukwaa la kuibua vipaji, kukuza ujuzi na kuwasaidia vijana kufikia malengo yao.
Benki ya CRDB pia inaandaa CRDB Bank International Marathon na kudhamini Ligi ya Shirikisho, Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu ya Taifa (Taifa Cup), baadhi ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi mbalimbali ndogo, ikiwemo CRDB Nanauka Cup.
Kupitia mashindano hayo, maelfu ya vijana hushiriki michezo na kupata fursa za kujipatia kipato.









