Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki na Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, amesema Kampuni ya PMM Tanzania Ltd imeonyesha meli tatu zitakazotumika katika kukuza biashara baina ya Tanzania na Oman.
Amesema kampuni hiyo itakuwa kiungo muhimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika sekta ya usafirishaji, hivyo kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi wa Taifa.
Balozi Kilima alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongozana na ujumbe wa Chemba ya Wafanyabiashara kutoka Oman, waliotembelea Kampuni ya PMM inayojishughulisha na usafirishaji na masuala ya madini.
“Tupo na wafanyabiashara kutoka Oman tangu Septemba 7, 2025 hadi leo tunapomaliza ratiba yetu. Tumekuja kuwaonesha uwezo wa kampuni zetu za ndani na kukuza biashara kati ya Tanzania na Oman. Huwezi kukuza biashara bila kuwa na usafiri wa uhakika, na PMM wameonyesha meli tatu ambazo zipo tayari kutumika katika kusafirisha bidhaa baina ya nchi hizi mbili,” alisema Balozi Kilima.

Aliongeza kuwa matarajio ya Serikali ni kuona ongezeko la biashara kati ya Tanzania na Oman, kupatikana kwa usafiri wa uhakika wa kupeleka bidhaa za Tanzania nchini Oman na kuingiza bidhaa za Oman nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa PMM Group, Dk. Judith Spendi, alisema ujio wa ujumbe huo ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kwani unafungua njia za kuuza bidhaa mbalimbali ikiwemo nyama ya mbuzi, nyama ya ng’ombe, chumvi, mboga na maua.
“Sisi kama wasafirishaji tunaona hii ni nafasi kubwa ya kukuza uchumi. Tutakuwa tukisafirisha makontena mengi ya bidhaa za Watanzania kwa meli zetu kwenda Oman, na kurudisha bidhaa zao kama mafuta na vifaa vya ujenzi vinavyohitajika hapa nchini,” alisema Dk. Spendi.
Aliongeza kuwa fursa zaidi zinapatikana kupitia uwekezaji kwenye bandari kavu, kilimo, viwanda vya uzalishaji wa dawa na maji, pamoja na utengenezaji wa mashine ambazo bado hazipo nchini.
Naye Salim Albusaidi, mmoja wa wafanyabiashara kutoka Oman, alisema siku tano walizotembelea miradi mbalimbali nchini zimewawezesha kuona fursa lukuki za kufanya biashara.
“Tumeona nafasi kwenye sekta za mboga, matunda, usafiri, utalii, madini, nyama, samaki na usindikaji wake. Tanzania tumeichagua kwa sababu tuna historia nzuri na tunathamini kinachofanyika hapa. Tayari baadhi ya mikataba tumeingia na tunafurahi kuona idadi ya wawekezaji inaongezeka,” alisema Albusaidi.
Aliongeza kuwa ujumbe huo unawakaribisha pia Watanzania kuwekeza nchini Oman, akibainisha kuwa fursa zipo wazi kwa sekta mbalimbali.




