Tuesday, March 3, 2026
spot_img
HomeAfyaSerikali yaja na mfumo mpya huduma jumuishi za VVU na NCDs

Serikali yaja na mfumo mpya huduma jumuishi za VVU na NCDs

Mtafiti Mkuu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. George Ruhago, amesema mapendekezo ya utekelezaji wa mfumo wa huduma jumuishi wa “moja kwa moja” kwa kuunganisha huduma za VVU/UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yanatarajiwa kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali.

Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu wa wadau wa afya uliofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 1, 2025, Prof. Ruhago amesema mfumo huo mpya utawawezesha wagonjwa kupata huduma zote muhimu kwa wakati mmoja, chini ya usimamizi wa timu moja ya kitabibu.

“Mfumo huu utamruhusu mgonjwa kutibiwa VVU, kisukari, shinikizo la damu na maradhi mengine katika kituo kimoja, bila kulazimika kuhudhuria kliniki tofauti. Huduma zitapatikana sehemu moja na kupitia mfumo mmoja wa uchunguzi na tiba,” amesema.

Ameeleza kuwa mkutano huo umekutanisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuboresha ramani ya utekelezaji, kushirikiana matokeo ya tafiti na kujadili mbinu za uendelevu katika rasilimali na utoaji huduma.

Prof. Ruhago ameongeza kuwa kipengele muhimu cha mfumo huu ni matumizi ya Activity-Based Costing and Management (ABC/M), mbinu inayotathmini gharama halisi za kila huduma ili kusaidia watunga sera kufanya maamuzi sahihi.

“Kwa kutumia ABC/M tunaweza kufuatilia kwa wakati halisi gharama na matokeo, jambo linalosaidia kugawa rasilimali kwa ufanisi zaidi na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.

Amesema hatua za awali za utekelezaji zitahusisha kuanzishwa kwa kliniki za huduma jumuishi katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na mapitio ya sera za malipo na fidia ili ziendane na mfumo huo.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Uchumi wa Afya, Dkt. Friday Ngaleson, amesema tafiti zinaonyesha kuwa kuunganisha huduma hakusababishi ongezeko kubwa la gharama, bali huboresha matokeo ya afya na kuongeza ufanisi.

“Huu si mabadiliko ya kiufundi pekee, bali mageuzi makubwa ya namna tunavyotoa huduma za afya,” amesema.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari wa Kisukari Tanzania (TDA), Prof. Kaushik Ramaiya, amesema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma kwa kuwa mgonjwa atahudumiwa na mtaalamu mmoja aliyehitimu, jambo litakaloboresha ufuatiliaji na matunzo ya afya kwa ujumla.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments