
Rais Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 10, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Kwa muhibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na TEC, huku yakijadili masuala mbalimbali ya kitaifa yanayoigusa jamii, ikiwemo siasa, imani na maendeleo, pamoja na umuhimu wa kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kujenga mustakabali mwema wa Taifa.


Aidha, mazungumzo hayo yamegusia nafasi ya madhehebu na viongozi wa dini katika kulea jamii yenye maadili mema, uwajibikaji na mshikamano, pamoja na mchango wao katika kuimarisha ustawi na maendeleo endelevu ya Taifa.
“Rais Samia amewashukuru Maaskofu hao kwa kuona umuhimu wa kukutana na kujadiliana naye masuala yenye tija kwa Taifa, akiwahakikishia dhamira yake ya kuendelea na utamaduni wa kushauriana na kushirikisha viongozi wa dini na makundi mbalimbali katika jamii kuhusu masuala muhimu ya kitaifa kila inapohitajika,”imeeleza taariga hiyo.






