HomeElimuMkuranga yapanua Shule kukabiliana na ongezeko la wanafunzi 

Mkuranga yapanua Shule kukabiliana na ongezeko la wanafunzi 

Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani imeanza mkakati wa kujenga shule za msingi na sekondari za ghorofa kwa kutumia mapato ya ndani, hatua inayolenga kuongeza nafasi za wanafunzi na kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Waziri Kombo, amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Sh bilioni 1.7 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Shule ya Sekondari Mwandege, huku ujenzi wa Shule ya Sekondari Muungano ukiwa pia sehemu ya mpango huo.

Amesema Sh bilioni 2.1 zinatumika katika ujenzi wa Shule ya Msingi Mwandege ya ghorofa yenye vyumba 16 vya madarasa, huku mchakato wa ujenzi wa shule hiyo ukiendelea na mkandarasi akiwa tayari amepatikana kwa ajili ya shule ya sekondari.

Kombo amesema miradi hiyo itagharamiwa kupitia vyanzo vya mapato vya ndani, ikiwemo eneo la maegesho ya malori lenye ukubwa wa ekari 50 pamoja na mapato yatakayopatikana kupitia upangishaji wa eneo la bandari kavu.

Amesema Halmashauri itaendelea kusimamia na kuimarisha vyanzo hivyo ili kupata fedha za kugharamia ujenzi wa miundombinu ya elimu.

Kwa mujibu wa Kombo, ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Mwandege unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Shule hiyo kwa sasa ina vyumba 12 vya madarasa, hivyo kukamilika kwa jengo jipya kutaongeza nafasi kwa idadi kubwa ya wanafunzi.

Amesema ongezeko la wanafunzi linatarajiwa kuwa kubwa kutokana na mabadiliko ya sera ya elimu, hivyo Halmashauri imejipanga kuongeza madarasa na kujenga shule mpya, hususan katika kata za Mwandege, Vikindu, Vianzi na Mipeko ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi.

Kombo amewataka wazazi na wadau wa elimu kushirikiana na Serikali kwa kuchangia mahitaji madogo ya shule, akisema Serikali inaendelea kugharamia elimu bila ada pamoja na mahitaji makuu ya uendeshaji.

Amesema lengo ni kuhakikisha wanafunzi wote watakaofaulu wanapata nafasi ya kuendelea na Kidato cha Kwanza, huku ujenzi wa shule za ghorofa ukitarajiwa kuongeza uwezo wa Halmashauri kuhudumia ongezeko hilo la wanafunzi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments