HomeBiasharaKivuko kipya kubeba abiria 300 Mafia

Kivuko kipya kubeba abiria 300 Mafia


PWANI:
 Serikali imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya cha Kilindoni Two, kinacholenga kupunguza changamoto ya usafiri kwa wakazi wa Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia katika eneo la Kimbiji, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, walipotembelea eneo kinapojengwa kivuko hicho.

Madiwani hao wameeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kivuko hicho, wakisema kukamilika kwake kutakuwa hatua muhimu katika kupunguza adha inayowakabili wakazi wa Mafia kutokana na kutegemea kivuko kimoja kwa usafiri wa majini.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Gulam Mohamed, ameishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi wa kisiwa hicho na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kingine.

Amesema kukamilika kwa kivuko hicho kutasaidia kuboresha usafiri wa kuingia na kutoka Mafia, hususan wakati kivuko kilichopo kinapopata hitilafu.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mafia, Mwanaisha Amer, ameihimiza Serikali kuhakikisha ujenzi wa kivuko hicho unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo.

Ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM kupitia hatua za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Mafia.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi huo, Mhandisi Faustin Lukindo, anayesimamia ujenzi wa kivuko hicho, amesema kazi imefikia asilimia 73 na inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Amesema kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 pamoja na tani 120 za mizigo, hatua itakayoongeza uwezo wa usafirishaji kati ya Mafia na maeneo mengine ya Tanzania Bara.

Mhandisi Lukindo amesema hadi sasa malipo ya asilimia 60 ya thamani ya mradi yamekwishalipwa.

Kwa muda mrefu, usafiri wa kuingia na kutoka Kisiwa cha Mafia umekuwa ukikabiliwa na changamoto kutokana na kuwepo kwa kivuko kimoja. Kivuko hicho kinapopata hitilafu, wananchi wengi hulazimika kuahirisha safari zao, huku baadhi wakitumia majahazi ambayo si salama kwa usafiri wa uhakika.

Kwa sasa, usafiri wa ndege ndio njia nyingine ya uhakika inayotumiwa na wasafiri wanaohitaji kuingia au kutoka Mafia.

Kukamilika kwa Kilindoni Two kunatarajiwa kuongeza uwezo wa usafiri wa majini, kupunguza utegemezi wa kivuko kimoja na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Mafia na Tanzania Bara.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments