HomeBiasharaAirtel yafanya ziara maalum kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi

Airtel yafanya ziara maalum kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi

Dodoma, Novemba 10, 2026 – Airtel Tanzania imesema itaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa binafsi za wateja wake ili kuendelea kutoa huduma bora na kuhakikisha usalama wa huduma zake za kidijitali.

Dhamira hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, wakati wa ziara ya heshima katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ambapo alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, pamoja na viongozi wengine.

Katika ziara hiyo, Kamoto aliishukuru Tume kwa mwongozo na ushirikiano iliowapatia katika kuendana na mfumo wa ulinzi wa taarifa binafsi, akieleza kuwa mafunzo na miongozo yaliyotolewa kwa wafanyakazi wa Airtel yamekuwa muhimu katika kuongeza uelewa wa namna sahihi ya kuchakata, kuhifadhi na kushughulikia taarifa za wateja.

Alisema ulinzi wa taarifa binafsi haupaswi kuonekana kama suala la kutimiza matakwa ya kisheria pekee, bali ni sehemu muhimu ya uendeshaji wa biashara na kujenga uhusiano wa muda mrefu na wateja.

“Kwa Airtel Tanzania, kulinda taarifa binafsi si wajibu wa kutimiza matakwa ya kisheria pekee, bali ni jukumu la msingi na sehemu muhimu ya namna tunavyoendesha biashara yetu. Kulinda taarifa za wateja ni muhimu katika kujenga na kudumisha imani pamoja na mahusiano ya muda mrefu,” alisema Kamoto.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika mafunzo na programu za uhamasishaji kwa wafanyakazi, pamoja na kuweka sera na mifumo ya ndani inayolenga kuhakikisha kuwa ulinzi wa taarifa binafsi unazingatiwa katika shughuli zake za kila siku.

Kamoto alisema hatua hizo ni muhimu zaidi wakati kampuni ikiendelea kupanua huduma zake za kidijitali na mipango ya ujumuishaji wa huduma za kifedha, hali inayoongeza umuhimu wa kutunza vyema taarifa za wateja ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kutembelea ofisi za Tume na kutambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Tume na sekta binafsi. Alisisitiza pia umuhimu wa makampuni mbalimbali kuelewa dhamira ya Tume, hususan katika kuhakikisha kuwa biashara zinaweka mifumo imara ya kulinda na kuhifadhi taarifa binafsi za wateja wao.

“Naipongeza Airtel Tanzania kwa utayari wake wa kushirikiana na Tume katika kuunga mkono utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuendeleza safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na fursa za kidijitali,” alisema Dkt. Mkilia.

Airtel Tanzania inathamini ushirikiano wake na Tume na inaendelea kujizatiti kuimarisha uhusiano huo katika kukuza usimamizi na utunzaji sahihi wa taarifa binafsi kwa lengo la kukuza na kujenga mazingira salama ya kidijitali nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments