Ubora wa ufuta unaozalishwa mkoani Pwani umeendelea kuchangia kuongezeka kwa bei katika minada, ambapo kilo moja imefikia Sh2,720 katika mnada wa sita uliofanyika katika Ghala Kuu la Kibiti.
Meneja wa CORECU Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, amesema bei hiyo imeongezeka ikilinganishwa na mnada wa tano, ambapo kilo moja iliuzwa kwa bei ya juu ya Sh2,500.
Amesema katika mnada wa sita zaidi ya tani 400 za ufuta ziliuzwa, huku bei ya chini ikiwa Sh2,370 kwa kilo. Aidha, hadi kufikia mnada wa tano, zaidi ya Sh bilioni 30 zilikuwa zimelipwa kwa wakulima.

Mantawela amewataka wakulima na wadau ambao bado wana ufuta majumbani kuufikisha katika maghala ili uweze kushiriki katika minada rasmi, akisema hatua hiyo inaweza kuongeza ushindani na kuchochea bei kupanda zaidi.
Amesema minada hiyo inaendeshwa kwa uwazi kwa kuwa wakulima wanapata fursa ya kufuatilia mchakato wa mauzo, huku akibainisha kuwa hadi kufikia mnada wa tano hakukuwa na mkulima aliyekuwa akidai malipo.
Kwa upande wa bei kwa wilaya, Mkuranga iliongoza kwa Sh2,720 kwa kilo, ikifuatiwa na Kibiti Sh2,673.12, Bagamoyo, Chalinze na Kisarawe Sh2,616, huku Rufiji ikiuzwa kwa Sh2,554.32.
Afisa Rasilimali Watu wa TMX, Haikael Mkongo, amesema mfumo wa kidijitali umeongeza uwazi katika mauzo kwa kumwezesha mnunuzi na mkulima kufuatilia bei ya zao hilo kupitia simu.
Amewataka wakulima ambao bado hawajapeleka ufuta kwenye maghala kufanya hivyo ili wanufaike na mfumo wa minada ya kidijitali, ambao pia huokoa muda kwa wakulima na wanunuzi.





