Marekani imetangaza kutosalimu amri kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), huku Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio akisema taasisi hiyo haina mamlaka kuhusu wananchi wala mfumo wa sheria wa nchi hiyo.
Rubio amesema Serikali ya Marekani imeanzisha kampeni ya kitaifa inayoshirikisha taasisi mbalimbali za umma ili kupinga kile ilichokiita hatua zisizo halali za ICC kuvuka mipaka ya mamlaka yake.
Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X, Rubio ametoa wito kwa mataifa mengine kuungana na Marekani kulinda mamlaka yao ya kitaifa dhidi ya kile alichodai kuwa tishio kwa uhuru wa nchi huru.
Amesema wananchi wa Marekani wana haki ya kuchagua viongozi wao, kutunga sheria zao na kusikilizwa kesi zao katika mahakama za nchi yao, jambo alilosema ni msingi wa utawala wa taifa hilo.
Rubio pia ameishutumu ICC kwa kupanua mamlaka yake kinyume na dhamira ya awali ya kuanzishwa kwake, akidai hatua hiyo inahatarisha mamlaka na uhuru wa mataifa yanayojitawala.




