HomeHabariTanzania kuwa mwenyeji wa mikutano ya UNFCCC

Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano ya UNFCCC

Tanzania imesaini mkataba wa uenyeji wa mikutano ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, Itifaki ya Kyoto na makubaliano ya Paris (UNFCCC) itakayokuwa ikifanyika Barani Afrika.

Tukio hilo ambalo ni la kihistoria, limeifanya Tanzania kuwa nchi pekee kusini mwa jangwa la Sahara kupata fursa hiyo ambayo itawezesha kuwa kinara wa jitihada za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akisaini mkataba huo Novemba 16, 2026, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema kufuatia kusainiwa kwa Mkataba huo Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mikutano miwili ya UNFCCC inayotarajia kufanyika februari 2027.

Ameitaja mikutano hiyo kuwa ni pamoja na Mkutano wa Kamati ya Watalaam wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Nchi zenye Uchumi wa chini na mkutano wa kamati ya watalaam kuhusu kujengea uwezo wa Nchi zinazoendelea chini ya Makubaliano ya Paris.

Ametaja manufaa inayotarajia kupata Tanzania kufuatia mkataba huo ni pamoja na Kuimarisha mahusiano ya Kidplomasia ya masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, kukuza utalii wa mikutano ya Kimataifa na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa.

Aidha Waziri Masauni ametaja faida nyingine kuwa ni kuongeza na kuvutia fursa za kiuchumi kwa wawekezaji wa Kitanzania na Kimataifa katika utoaji wa huduma zitakazoambatana na Mikutano hiyo.

“Mkataba huu ni udhibitisho wa kukubalika kwa juhudi zinazofanywa na Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha diplomasia ya masuala ya mazingira pamoja na imani ya nchi yetu kuongoza mikutano mikubwa” amesema Mhandisi Masauni.

Waziri Masauni amesema kufuatia Nchi ya Eithiopia kuteuliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa COP 32, upo uwezekano wa baadhi ya mikutano na shughuli za maandalizi kufanyika Tanzania na kuwezesha kunufaika na fursa za kiuchumi, diplomasia na teknolojia.

Kufuatia hatua hiyo, Mhandisi Masauni amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi na wadau wengine kujiandaa vyema na kujiimarisha katika uwezo wa utoaji huduma na kuweka mazingira rafiki kwa mikutano ya kimataifa.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 1992, Itifaki ya kyoto ya mwaka 1997 na Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015.

Mikataba hii pamoja na mambo mengine inatoa utaratibu wa Nchi Wanachama kutimiza wajibu wao wa kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kunufaika na miradi ya biashara ya kaboni.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments