Tuesday, May 5, 2026
spot_img
HomeHabariPolisi Morogoro wamsaka mtuhumiwa kwa kumuua mkewe

Polisi Morogoro wamsaka mtuhumiwa kwa kumuua mkewe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamtafuta Helakumi Kacheri kwa tuhuma za kumuua mkewe katika tukio lililotokea Januari 4, 2026 mchana, katika Kitongoji cha Tindegela, Kata ya Singisa, Wilaya ya Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, mtuhumiwa anadaiwa kumshambulia marehemu kwa kutumia silaha yenye ncha kali, na kumsababishia majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufariki dunia. Inadaiwa chanzo cha tukio hilo ni wivu, baada ya mtuhumiwa kumtuhumu marehemu kuendeleza mahusiano ya karibu na mzazi mwenzake wa awali. Baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka eneo la tukio na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendelea kufanya uchunguzi wa matukio mawili tofauti ya vifo yaliyotokea katika wilaya za Kilombero na Mvomero.

Tukio la kwanza limetokea Januari 4, 2026 asubuhi, katika Kitongoji cha Isago, Kata ya Mngeta, Wilaya ya Kilombero, ambapo Jese Melumba (49), mkulima na mkazi wa Isago, alifariki dunia kwa tuhuma za kunywa sumu ya kuulia magugu ya shambani. Uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa mabaki ya dawa ya kuulia magugu aina ya Banafos, hali inayozidisha mashaka kuwa marehemu alijiua kwa kunywa sumu hiyo.

Tukio jingine limeripotiwa kutokea Januari 3, 2026, katika Kitongoji cha Doma Stand, Kijiji na Kata ya Doma, Wilaya ya Mvomero, ambapo Ally Charles Dagaza (38), mkulima na mkazi wa Doma, alifariki dunia akiwa shambani kwake baada ya kukanyagwa na mnyama Tembo. Inadaiwa marehemu alikuwa analinda miche ya nyanya na zao la pilipili wakati tukio hilo linatokea.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi wa matukio hayo pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa anayesakwa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments