Uchomaji wa nguzo na wizi wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Iringa na Njombe umesababisha kukatika kwa huduma katika maeneo yaliyoathirika, kuathiri shughuli za wananchi na kuisababishia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) hasara.
Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ya shirika hilo, Oktoba 28, 2026, TANESCO imesema vitendo hivyo vinahusisha uchomaji wa nguzo, uharibifu wa nyaya na wizi wa transfoma, hali inayotishia upatikanaji wa huduma ya umeme kwa uhakika.
Mkoa wa Njombe umeathirika kwa kuungua kwa nguzo 66 katika maeneo ya Yakobi, Iboya, Utalingolo, Image, Utengule, Igoma, Makete, Ikonda, Ilela, Ipelele, Lupila na Mgala. Aidha, transfoma moja imeibwa katika eneo la Mafinga, Wilaya ya Wanging’ombe.
Kwa upande wa Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Kilolo imeripoti kuungua kwa nguzo 10, kuharibika kwa nyaya na kuibwa kwa transfoma moja yenye uwezo wa kVA 100.
Wilaya ya Mafinga nayo imeripoti kuungua kwa nguzo tano na kuibwa kwa transfoma mbili, kila moja ikiwa na uwezo wa kVA 50.
Kutokana na hali hiyo, TANESCO imekemea vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya umeme na kuwataka wanaohusika kuacha mara moja. Shirika hilo pia limewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapochoma moto kwa ajili ya shughuli za kilimo na kusafisha mashamba ili kuzuia moto kusambaa na kuharibu nguzo za umeme.
Aidha, TANESCO imehimiza wananchi kushirikiana kulinda miundombinu hiyo kwa kutoa taarifa kuhusu wizi, uchomaji wa makusudi na uharibifu wa vifaa vya umeme kwa Jeshi la Polisi au kupitia namba ya huduma kwa wateja ya shirika hilo, 180, ili hatua stahiki zichukuliwe.






