Thursday, March 5, 2026
spot_img
HomeAfyaWizara yazindua operesheni kupambana na ndoa za utotoni na kukatisha masomo

Wizara yazindua operesheni kupambana na ndoa za utotoni na kukatisha masomo

Msimu wa kufunguliwa kwa shule umefika, lakini bado tunaendelea kupokea taarifa nyingi za watoto wa kike kutoroshwa kutoka kwenye masomo ili kuolewa bila ridhaa yao. Hii ni hali inayokiuka haki zao na pia ni kinyume cha sheria, hasa kwa kuwa watoto hawa bado wako katika umri usioruhusu ndoa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kote nchini, imejizatiti kuhakikisha kuwa haitakubali vitendo vya aina hiyo. Tutaendelea kufuatilia kila mtuhumiwa anayetajwa, kuanzia mshenga, wanaume wanaoolewa, waozaji wa mahari, wapokeaji mahari, ndugu, jamaa, na marafiki waliopo katika mchakato huu haramu.

Natoa angalizo kali na onyo mapema kwa wote wanaohusika ili kuepuka madhara makubwa. Tayari operesheni za kusimamia sheria hizi zinaendelea kwa nguvu, zikiendeshwa na Wahe Wakuu wa Wilaya, Mikoa, na madawati ya jinsia katika maeneo mbalimbali nchini. Tumeanzisha mkakati wa kuwafikia wote walioko katika mchakato huu ili kuhakikisha haki inapatikana.

Tunawaomba wananchi wote kuendelea kutuma taarifa zinazohusu vitendo hivi, kwani hakika kila mmoja atafikiwa popote alipo. Lengo letu kuu ni kuhakikisha watoto wa kike wanaendelea na masomo yao, wakatimize ndoto zao, na kuwa na maisha bora bila kukataliwa haki zao za kisheria.

Kwa mawasiliano na usaidizi zaidi, wananchi wanaweza kutuma ujumbe kwa nambari ya simu 0765 345777 ambapo tutaanza hatua za kuchukua hatua mara moja.

Ndugu wanahabari, napenda kuwashukuru kwa ushirikiano wenu mkubwa. Tunaomba tuendelee kushirikiana kikamilifu ili kuwalinda watoto wetu wa kike dhidi ya ndoa za utotoni na kukatishwa masomo kwa sababu ya ndoa zisizo halali na zisizokubalika kisheria.

Wizara na wadau wote tunaungana kutoa tamko thabiti la elimu na ulinzi wa haki za watoto katika suala hili muhimu.

Ahsanteni sana.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments