Watanzania hawatalazimika tena kusubiri kwa miezi kadhaa kupata magari ya pick-up na magari mengine mepesi ya biashara yanayoagizwa kutoka nje baada ya Kampuni ya Saturn Corporation kupanua kiwanda chake cha kuunganisha magari kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Kampuni hiyo imezindua rasmi upanuzi wa kiwanda hicho ambao sasa utawezesha kuunganishwa hapa nchini kwa magari ya pick-up pamoja na magari mengine mepesi ya biashara, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa katika sekta ya utengenezaji magari nchini Tanzania.
Uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Saturn Corporation wa kuunga mkono agenda ya serikali ya viwanda kwa kuongeza ajira, kuharakisha uhamishaji wa teknolojia na kupunguza muda wa kusubiri magari kwa wateja wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.
Moja ya vivutio vikubwa katika hafla hiyo ilikuwa uzinduzi wa gari la Sinotruk Bolden pick-up lililounganishwa hapa nchini, hatua iliyoonesha uwezo wa Tanzania kuzalisha magari ya kisasa yanayokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Judith Kapinga, aliipongeza Saturn Corporation kwa mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa ndani, utoaji wa ajira na maendeleo ya ujuzi kwa Watanzania.
“Nimefurahishwa na mafanikio makubwa ambayo Saturn Corporation imeyapata ndani ya kipindi cha miaka miwili pekee. Ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zilizowanufaisha zaidi ya Watanzania 2,800 ni mchango mkubwa kwa uchumi wetu na agenda ya serikali ya viwanda,” alisema Kapinga.
Waziri huyo alizindua rasmi kiwanda hicho kilichopanuliwa katika hafla iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka miwili tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho Kigamboni. Tangu kuanza shughuli zake, kampuni hiyo imekuwa ikijikita zaidi katika kuunganisha magari makubwa ya biashara yanayotumika kwenye sekta za migodi, ujenzi, usafirishaji na miradi ya miundombinu.
Upanuzi huo sasa unaifungulia kampuni hiyo soko jipya la magari ya pick-up na magari mepesi ya biashara ambalo linaendelea kukua kwa kasi nchini.
Mkurugenzi wa Saturn Corporation, Rahimtullah Habib, alisema uwekezaji huo unaonesha imani kubwa ya kampuni hiyo katika mustakabali wa viwanda nchini Tanzania pamoja na dhamira ya kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani.
“Tunataka kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya viwanda nchini huku tukikidhi ongezeko la mahitaji ya magari bora yanayounganishwa hapa nchini. Uzalishaji wa ndani unasaidia kuongeza ajira, kukuza ujuzi wa kitaalamu, kuhamisha teknolojia na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Habib.
Aidha, aliiomba serikali kuendelea kuboresha sera zinazounga mkono uunganishaji wa magari nchini ikiwemo mazingira bora ya kodi kwa magari yanayounganishwa hapa nchini, kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani na kuboresha ufanisi bandarini ili kurahisisha upatikanaji wa vipuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vinmart Group, Chetan Chug, alisema uwekezaji huo unaonesha imani ya muda mrefu waliyonayo kwa uchumi wa Tanzania na mazingira yake ya uwekezaji.
Saturn Corporation pia ilisaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati na Sinotruk yatakayosaidia kuongeza ushirikiano wa kiufundi na kuimarisha uzalishaji wa magari mbalimbali hapa nchini.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Saturn Corporation imekua kwa kasi na kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka magari 10 hadi magari 30 kwa siku, huku zaidi ya Watanzania 360 wakiajiriwa moja kwa moja katika shughuli za uunganishaji, uhandisi na uzalishaji.
Kampuni hiyo pia imeendelea kutoa mafunzo kwa wahandisi na mafundi wa Kitanzania ili kuwajengea uwezo wa kimataifa pamoja na kuimarisha ushirikiano na vyuo vya ufundi nchini.
Mbali na hilo, Saturn Corporation imetangaza mpango wa kuanza kuunganisha magari yanayotumia gesi asilia (CNG) ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono usafiri safi na nafuu nchini Tanzania.




